DR. TULIA APEWA ULEZI WA WATOTO WA KITUO CHA JERUSALEM KIMARA KKKT

 

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dr. Tulia Ackson leo December 6, 2020 amepewa kuwa mama mlezi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Jerusalem kinachosimamiwa na kanisa la KKKT Kimara. 

 

Akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa la KKKT usharika wa Kimara jijini Dar es Salaam, Mchungaji Kiongozi, Wilbrod Mastai amesema kuwa mbali na Mheshimiwa Dr. Tulia kuwa mlezi wa kituo hicho wameamua kumpa kuwa mzazi wa hao watoto. 

 

"Tumeamua kumpa heshima ya pekee ya kuwa mzazi wa watoto 21 wa kituo chetu cha kulelea watoto Yatima kinachosimamiwa na kanisa letu, hivyo tunamshukuru kwa kuweza kukubali ombi letu" 

 

Katika tukio lililovuta hisia za waumini ni kubatizwa kwa mtoto mmoja kati ya hao 21 Meshack Elinaza ambaye anawiki mbili tokea amepokelewa kituoni hapo.

 

 Kwa upande wa Dr. Tulia Ackson ameshukuru uongozi wa kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Kimara kwa kuweza kumpa heshima ya kuwa mama wa watoto hao, huku akiahidi kuwalea katika maadili ya kidini na kuweza kumjua Mungu. 

 

"Niwashukuru kwa kunipa heshima ya pekee kwasasa nitakuwa nanyi bega kwa bega katika kuwalea watoto hawa waliopo kituo chenu, sina mengi zaidi kuzidi kushukuru na mzidi kuniombea ili niweze kuwa mama bora,"-Dr. Tulia Ackson