Harusi yashindwa kufungwa"Bwana harusi aingia mitini Mbeya"
Na Ezekiel Kamanga,Mbeya
Katika hali isiyo ya kawaida Bwana harusi ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la New Hope Mountain(NHM) Yusuph Asagwile Mwakasole mkazi wa Mtaa wa Ilembo Kata ya Iyela Jijini Mbeya ametoroka na kumtelejeza bibi harusi aitwaye Dorcus Jonas ambaye alitarajia kufunga naye ndoa katika Kanisa la Pentecoste Revival lililopo Iyela disemba 23,2020.
Akielezea kisa hiki Balozi wa Mtaa wa Ilembo Alice Mwanangwa alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baba wa bwana harusi Asagwile Mwakasole aliyedai Mchungaji Enock Mgogo wa Kanisa la Pentecoste Revival kusitisha harusi akidai bwana na bibi harusi hawawezi kufunga ndoa kwa kuwa maharusi wamezini kabla ya kufungishwa ndoa.
Baada ya balozi kukosa majibu sahihi aliamua kutoa taarifa kituo cha Polisi Mwanjelwa kutokana na kuwepo habari za kusadikika kuwepo kwa kijana aliyehusika kumtorosha bwana harusi kumpeleka Dar es Salaam na sasa kufanya jaribio la kumtorosha bibi harusi ili waungane naye huko.
Hata hivyo balozi baada ya kubaini njama ovu hizo kwa kushirikiana na familia ya bwana harusi walifanikiwa kumkamata kijana huyo jina linahifadhiwa ambaye alikiri kuhusika na tukio hilo akidai kutumwa na Askofu wao aliyeko Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake bibi harusi Dorcus Jonas alisema hivi karibuni alipigiwa simu na mama askofu wa jijini Dar es Salaam aliyedai ameoneshwa kuwa yeye na mchumba wake Yusuph wameanguka hivyo wanapaswa kuongozwa sala ya toba kwa kuwa wamezini kauli ambayo bibi harusi alipinga maono hayo.
Aidha alisikitishwa na kitendo cha mama askofu kumtuhumu kuwa amezini wakati si kweli ingawa alizidi kumshinikiza.
Hata hivyo mama askofu alimwambia bibi harusi kuwa bwana harusi amekiri kuzini hivyo naye akubali ili aende Dar es Salaam watengeneze na waache huduma iliyopo Mbeya waanze maisha mapya jambo ambalo Dorcus alikataa na kushikilia msimamo wa kutozini na mchumba wake.
Akisimulia kisa hiki huku akibubujikwa na machozi Dorcus alishangazwa na kitendo cha mchumba wake kukata mawasiliano na kutorokea kusiko julikana ilhali taratibu zote za kufunga ndoa zikiwa zimekamilika sambamba na shela,viatu na nguo za kubalisha ukumbini siku ya harusi ambayocilikuwa ifungwe disemba 23 mwaka huu.
Alisema kama kulikuwa na kizuizi katika kanisa hilo iweje atoroke bila mawasiliano yoyote akijua maandalizi yote yakiwa yamekamilika kupitia kamati ya harusi.
Kwa upande wake mjomba wa bibi harusi na mlezi wake Sadiki Cornel Mwakihaba alisema kitendo kilichotokea kwa binti yao kimempa fedheha kwani kama familia walipokea michango ya watu na taratibu za kumuaga zilifanyika.
Naye baba mzazi wa bwana harusi Asagwile Mwakasole alisema kijana aliyemtorosha mtoto wake ahojiwe vizuri ili aeleze aliko mtoto wao.
Hata hivyo kaka wa bwana harusi Joel Mwakasole alisema kwa kushirikiana na Polisi walifanikiwa kumkamata kijana mmoja anayetuhumiwa kumtorosha bwana harusi na kujaribu kumtorosha bibi harusi.
Joel alisema baada ya mahojiano alikiri kuhusika kumtorosha bwana harusi kwa kile alichodai ni agizo kutoka kwa askofu wao anayeishi Dar es Salaam.
Enock Mgogo ni mchungaji wa Kanisa la Pentecoste Revival lililopo Ilembo Kata ya Iyela alisema yeye aliombwa tu kufungisha ndoa katika kanisa lake kwa kuwa kanisa la bwana harusi halina kibali cha kufungisha ndoa.
"Nilipata taarifa kwa askofu kuwa vijana hao wamezini hivyo usifungishe ndoa hiyo nami nikatii kwa kuwa niliombwa tu kufungisha"alisema mchungaji Mgogo.
Mgogo alisema binti ni muumini wake na alipomuuliza tuhuma za kuzini na mchumba wake alikataa.
Mchungaji Mgogo alisema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika kanisa lake.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya maandalizi ya sherehe Judith Mgeyekwa alisema kamati ilikamilisha manunuzi ya kila kitu hivyo hawana pesa za kuwarejeshea walichangia harusi hivyo hivyo wanamsubiria bwana harusi atejee ili ndoa ifungwe kama si kanisani basi hata serikalini.
Judith alisikitishwa na kitendo cha mchungaji Mgogo kutotoa taarifa za kusitisha kufungwa ndoa licha ya kamati kumshirikisha kila jambo katika maandalizi.
0 Comments
Post a Comment