WAFAMASI WAKUMBUSHWA KUHUISHA LESENI ZAO KABLA MWAKA KUISHA


Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma


Wafamasia, fundi dawa sanifu na wasaidizi nchini wamekumbushwa kuhuisha leseni zao kabla ya tarehe 31 Disemba mwaka huu ili waweze kuendelea kufanya kazi za kitaaluma kwa mwaka unaokuja.


Wito huo umetolewa leo na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe wakati akiongea na afisa habari wa Wizara ya Afya,ofisini kwake jijini Dodoma.


Bi. Elizabeth amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu Namba 22 cha Sheria ya Famasi, Sura 311 kinawataka wafamasia kuweza kuhuisha majina yao kwenye rejista kwa utaratibu maalamu.


"Pamoja na baraza la famasi kuwasajili wanataaluma kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya famasi nchini,kifungu kinatutaka kabla ya tarehe 31 Desemba ya kila mwaka kuhuisha majina ili kuweza kufanya kazi  za kitaalam kwa mwaka unaokuja".Alisisitiza Msajili


Kwa upande wa uuzaji wa dawa Msajili wa Baraza hilo Bi.Shekalaghe amesema  tatizo la uuzaji wa dawa kiholela limekuwa ni tatizo sugu hapa nchini na hivyo mwaka huu Waziri wa Afya ameidhinisha kanuni za udhibiti na usimamizi wa uuzaji wa dawa za cheti na hivyo amewataka wanataaluma wa famasi kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa kanuni hizo.


"Kama wafamasia na wataalam tukumbuke tuna watu tunawasimamia na kuhakikisha dawa tunazitoa kwa kuzingatia miongozo iliyopo na Baraza halitosita kumchukulia hatua yeyote atakayeenda kinyume na kanuni hizo".Aliongeza Bi. Shekalaghe.


Mbali na hayo Bi. Shekalaghe amewataka wananchi  kutoa taarifa kwenye Baraza hilo pale wasiporidhika na huduma zitolewazo katika Famasi na maduka ya dawa muhimu kwa kupiga 0736 222 504 au namba bila malipo 0800110015 ili waweze kutatua changamoto wanazozipata wakati wanapatiwa huduma hizo. 

-MWISHO-