AJENDA YA UANZISHWAJI WILAYA MPYA JIJI LA MBEYA YATEKA KIKAO CHA KWANZA BARAZA LA MADIWANI

Na Ripota wa Mbeya Yetu

Ziara ya Kampeni ya Rais Dkt John Pombe Magufuli Septemba 30 Jijini Mbeya ndiyo ambayo imeanzisha mchakato wa kugawanywa kwa Wilaya mbili ndani ya Jiji la Mbeya.

Rais Magufuli alizingatia vipaumbele


vinavyoshabihiana na ukubwa wa Jiji la idadi ya watu wake ili kusogeza karibu huduma za maendeleo kwa wakazi wa Jiji la Mbeya.

Aidha katika ziara yake Dkt Magufuli alishauri kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Mbeya kichukue jambo hili kama kipaumbele cha kwanza ili utekelezaji uanze mara moja.

Katika kikao chake cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Mbeya Ijumaa Januari 29, 2021, Baraza la Madiwani kwa pamoja wamepitisha na kuridhia kuanzishwa kwa mchakato wa kuanzishwa kwa Wilaya mbili za Jiji hilo.

Chini ya Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dormohamed Issa na Katibu wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Amede Ng’wanidako kikao kimeridhia kwa pamoja uanzishwaji wa Wilaya mpya itakayotokana na Wilaya moja ya Mbeya Mjini.

Akisoma taarifa ya uanzishwaji wa Wilaya mpya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Amede Ng’wanidako amesema ajenda hiyo imetokana na agizo la Rais  Magufuli ambapo mchakato wa utekelezaji wake unaanzia kwa kikao hicho cha kwanza cha Baraza la Madiwani.

Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Dormohamed Issa amesema kuwa kuanzishwa kwa wilaya mpya itakayotokana na Wilaya moja ya Mbeya mjini itasaidia kusogeza maendeleo na kuwa Baraza la Madiwani wa Jiji la Mbeya limeridhia uanzishwaji wake.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi Mariam Mtunguja amesema kuwa hatua ya uanzishwaji wa wilaya mpya itafuatiwa na maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo wananchi,Viongozi wa dini na Wazee wa Kimila.

‘’Baraza limepokea maagizo ya Rais na huu ndio utekelezaji wake, lengo ni kusogeza karib u huduma kwa wananchi katika sekta za elimu afya na Miundo mbinu’’amesema Bi Mtunguja.