DKT TULIA AZIDI KUMALIZA UKATA WA VIJANA JIJINI MBEYA,

-Akabidhi Bodaboda na Bajaji za Sh Mil 62

Na Ripota wa Mbeya Yetu

‘’Tulikuwa tunakodishwa Bajaji kwa siku tunapeleka malengo kwa Bosi, siku nisipofikisha malengo nahofia kunyang’anywa Bajaji anakabidhiwa dereva mwingine…sasa hivi hofu hiyo itatoweka, namiliki Bajaji yangu  mwenyewe mali yangu nitarejesha mkopo wangu Tulia Trust’’.


Ndivyo ambavyo amesikika kijana mmoja mwendesha Bajaji kutoka Jijini Mbeya akidhihirisha furaha yake baada ya kukabidhiwa Bajaji kutoka Taasisi ya Tulia Trust Januari 21,2021,zoezi ambalo limefanyika Stand ya Daladala Kabwe Jijini Mbeya  likiwezeshwa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson.

Hizi ni harakati za kuwakwamua vijana ili kuwezeshwa kujiajiri linalofanywa na Naibu Spika Dkt Tulia Ackson ambaye pia ndiye Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini katika kuhakikisha vijana wengi ambao awali walikuwa ni wazururaji wasio kuwa na kazi maalumu wanajiajiri.


Jumla ya Bajaji 5 na Pikipiki 10 zenye thamani ya Tsh Mil 62 zimekopeshwa na Taasisi ya Tulia Trust kwa Chama cha Bajaji na Bodaboda  Mbeya mjini kwa lengo la kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wakati wa makabidhiano hayo katika kituo cha Daladala cha Kabwe Dkt Tulia amesema kuwa  Taasisi ya Tulia Trust ipo kwa nia ya kuyawezesha makundi ya vijana kujikwamua kiuchumi.

                                                   

‘’Leo hii tunakabidhi Vijana Pikipiki 10 na Bajaji 5 zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi, kuongeza uzalishaji ili kuendesha maisha yao ya kila siku’’amesema Dkt Tulia.

Dkt Tulia amefafanua kuwa muendelezo huo wa mikopo umefuatia marejesho ya wakopaji wa awali ambao wamerejesha mikopo yao kwa wakati na hivyo kusaidia wengine kukopeshwa.

                                                 

Amesema kuwa baadhi ya watu hudhani kuwa  mikopo hiyo inapotolewa hadharani kuna  baadhi ya makundi yamesahaulika bali amefafanua kuwa mikopo hiyo huwagusa watu aina zote wakiwemo wale wanaofika moja kwa moja ofisini yakiwemo makundi ya                                                       akina mama.                            .                                                        

Kadhalika Dkt Tulia amezidi kusisitiza na kuwaomba wakazi wa Jiji la Mbeya kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kuepuka gharama kubwa kwenye matibabu wakati wanapougua.

                                                    

AmesemaTaasisi ya Tulia Trust kwa kushirikiana na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeanzisha utaratibu wa kumuwezesha mwananchi mmoja mmoja kuchangia kiasi cha Tsh 30,000/- kwa mwaka  ambayo inawekezekana kuchangia Tsh 100/- kila siku ambayo baada ya wiki moja hukabidhiwa kadi yake ya Bima ya Afya.