Mbunge wa Lupa Chunya Masache Njelu Kasaka akizindua wiki ya Upandaji Miti Wilayani Chunya Mkoani Mbeya


Na Ripota wa Mbeya Yetu

Mbunge wa Jimbo la Lupa Wilayani Chunya Mkoani Mbeya Mhe.Masache Njelu Kasaka leo amezindua kampeni maalumu ya Wiki ya Kupanda Miti ikiwa ni mpango wa Kitaifa kukabiliana na ukame na Uhifadhi wa Mazingira.

 Kasaka ambaye amekuwa mgeni rasmi katika kampeni hiyo Wilayani Chunya ameshiriki kikamilifu upandaji miti katika maeneo mbalimbali na kuwataka wanajamii kujenga nidhamu ya kupanda miti kuihifadhi na kuitunza.

‘’Tupande Miti ili itusaidie kuondokana na ukame na kuleta mvua, kila mwananchi aguswe na zoezi hili tujijengee tabia hii tusisubiri wakati wa kampeni ya wiki ya upandaji miti’’.

Amesema Chunya ni moja kati ya wilaya zilizojaaliwa kuwa na misitu mikubwa ya asili lakini kumekuwa na uharibifu wa uvunaji holela wa mbao za mining na uchomaji wa mkaa hivyo amewataka wanajamii kushirikiana kwa pamoja kulinda mazao yatokanayo na misitu ya asili.

Ameendelea kusema kuwa wilaya ya Chunya ni moja kati ya wilaya zinazozalisha tumbaku ambapo asilimia kubwa ya wakulima hukata miti kwa ajili ya kuni za kuchomea tumbaku na kuwa iwapo wananchi hawatapanda miti kuna hatari kubwa ya  Chunya kugeuka kuwa jangwa.

‘’Panda Mti Kata mti haitoshi….tupande miti mitano tukate mti mmoja itatusaidia kulinda na kuihifadhi misitu yetu’’amesema Kasaka.