Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Breg. Jen. Nicodemus Mwangela amemuomba Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa Mamlaka ya Maji ya Vwawa na Mlowo kwa kukosa ubunifu wa kazi ya kuwapelekea wananchi maji.

Mkuu wa Mkoa amemwambia Naibu Waziri alipofanya ziara Mkoa wa Songwe leo 5 Januari 2021 ya kukagua miradi ya maji.

"Mamlaka hii bado haijakidhi mahitaji kwa wananchi pamoja na Mhe. Rais, Dkt Magufuli kuleta fedha za kununua pampu kwenye mradi wa Vwawa lakini bado maji wananchi hawapati" Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Mwangela.

Aidhaa, Mamlaka hii ina matatizo ya kutoa bili ya maji mfano Kaya moja inapelekewa bili ya maji ya Shilingi 20,000 au 30,000 kwa mwezi lakini sehemu za kambi kama Jeshi la Polisi na Magereza ambapo matumizi ya maji ni makubwa wanapewa bili ya shilingi 3,000 tu kwa mwezi sasa sisi tunaona uongozi wa Mamlaka hautufai katika kuhudumia wananchi.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amechukua hatua ya kumsimamisha Kazi Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Vwawa na Mlowo.

Wakati huo huo Naibu Waziri amesema ndani ya miezi sita Mkoa wa Songwe utaona mabadiliko chanya Makubwa kwenye sekta ya maji.