SIMULIZI YA KUSIKITISHA YA WAHABESHI 61 WALIONASWA MBEYA WAKIELEKEA SAUZI

Vijana hawa wapatao 61 ni raia wa nchini Ethiopia waliokuwa wamelundikana ndani ya Lori wakisafirishwa usiku na mchana wakikimbia nchini kwao kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika.

Safari yao ya muda mrefu ilikuwa inakaribia ukingoni, wametoka nchini kwao Ethiopia na kupita Somalia kisha kuvuka nchini Kenya na hatimaye kuingia Tanzania kupitia Arusha.

Wamevuka vizuizi vingi wakipitia katika barabara kuu za miji mikubwa ya nchi hii kama vile Namanga Arusha Kilimanjaro,Horohoro Tanga,Morogoro,Iringa, Njombe na Jiji la Mbeya wakiwa wamefungiwa ndani ya lori hili  nambari T 509 AZZ kama mizigo.

Matumaini ya safari yao kufikia ukingoni yamekomea katika kijiji cha Garijembe Barabara Kuu ya Tanzania –Malawi huko Mbeya vijijini zikiwa zimebaki kilomita chache tu kuvuka mpaka wa Tanzania na Malawi.

Mnamo majira ya saa tano usiku Januari 12 katika kizuizi cha ukaguzi wa Jeshi la Polisi eneo la Garijembe vijana hawa, wengi wao wakiwa ni vijana wadogo  wenye umri kati ya miaka 18 na 20 waliamriwa kushuka katika Lori hili.

Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Jerome Ngowi ni kwamba kulikuwa na mabishano kidogo na dereva wa gari hilo Badri Ramadhani kabla ya kufunguliwa kwa mlango wa nyuma wa Lori hilo.

Inaelezwa kuwa Dereva huyo alijaribu kuwashawishi askari polisi kwa kutaka kutoa rushwa ya Shilingi Milioni 30 ili awaruhusu kuvuka kizuizi hicho ambacho iwapo tu wangefanikiwa vijana hao 61 wangekuwa wamevuka mpaka wa Kasumulu kuelekea nchini Malawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Jerome Ngowi anasema mara baada ya kufunguliwa kwa kufuri za mlango wa nyuma wa Lori hilo ndipo lilipojitokeza kundi kubwa la vijana raia wa nchini Ethiopia wakiwa wamechoka kwa njaa na kiu na kushuka ndani ya Lori hilo ambalo halikuwa hata na madirisha.

Kamanda Ngowi amebainisha kuwa awali katika mahojiano na dereva wa gari hilo alidai kuwa amepakia bidhaa mbalimbali za dukani lakini baada ya kuamriwa kufungua mlango wa nyuma wa gari ndipo ilipobainika kuwa amepakia wahamiaji haramu waliokuwa wakielekea Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi.

Kutokana na tukio hilo Kamanda Ngowi amesema kuwa gari lililotumika kusafirisha wahamiaji haramu ambalo lina anuani ya mmiliki wake Mwanaidi Idd Kishavi wa Jijini Arusha litataifishwa na kuwa mali ya serikali.


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Jerome Ngowi ametoa wito kwa wasafirishaji wa wahamiaji haramu kujiepusha na biashara hiyo ya binadamu kwa kuwa ni kinyume cha sheria za Kimataifa na hata maadili ya dini.

TAMATI.