Mhandisi Maryprisca: ‘’HAKIKISHENI MKANDARASI ANAREJESHA PAMPU
YA MAJI MRADI WA NYAMTUKUZA’’
Na Ripota wa Mbeya Yetu, Mwanza
Naibu Waziri wa Maji,Mhandisi MaryPrisca Mahundi (Mb) amemuagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita Mhandisi
Frank Changawa kuhakikisha mkandarasi wa awali aliyekuwa anatekeleza mradi wa
Nyamtukuza Petty and Company (Ltd), kurejesha pampu ya mradi huo aliyorudishiwa
kwa ajili ya matengenezo madogo ili iweze kufungwa na wananchi waendee kupata
huduma ya majisafi na salama.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa anakagua utekelezaji wa mradi huo
ambao umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na wakandarasi kushindwa
kukamilisha mradi kwa wakati hadi mkataba ulipovunjwa na kazi ya utekelezaji
kuchukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA).
“Ninawapa siku saba (GEUWASA) kuhakikisha pampu iliyochukuliwa
na Mkandarasi kwa ajili ya matengenezo inarejeshwa haraka ili ije ifungwe
kwenye mradi kama mchoro wa awali unavyoonesha kufunga pampu mbili ili moja
ikipata hitilafu, basi nyingine iendelee kufanya kazi, wananchi waendelee
kupata huduma ya maji”, amesema Mhandisi Mahundi, na kusisitiza kuwa ndani ya
siku hizo saba kupatiwa ripoti ya pampu hiyo kama imerejeshwa.
Amesema wananchi wengi nchini hususani wa maeneo ya
vijijini wanahitaji maji na hivyo kuwataka watekelezaji wa miradi hiyo
kukamilisha kwa wakati unaotakiwa ili wananchi wapate huduma wanayostahiki.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) na watendaji wake kwa kuweza kutekeleza
mradi huu ambao hapo awali ulikuwa kati ya miradi kichefuchefu kwa kutokamilika
kwa wakati na sasa mradi umefikia hatua za mwisho na baadhi ya wananchi wa
Nyamtukuza wameanza kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.
Mradi wa Nyamtukuza kwa sasa unatekelezwa na GEUWASA kwa kutumia
wataalam wa ndani (Force Account) na umegharimu shilingi bilioni 11 ambapo kwa
kutumia watalaamu hao wa ndani serikali imeweza kuokoa shilingi bilioni 4 na
unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi machi, 2021.
0 Comments
Post a Comment