MHANDISI MARYPRISCA AKUNJUA MAKUCHA AAGIZA KUTUMBILIWA FUNDI WA MIUNDO MBINU.

Ziara ya Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi Mkoani Manyara imesababisha fundi wa Miundo mbinu Amos Abi kukaa mguu nje mguu ndani.

Mhandisi Maryprisca amebaini hujuma dhidi ya jitihada za serikali za kumtua Ndoo Mama Kichwani zikishindwa kutekelezwa ipasavyo baada ya baadhi ya vituo kushindwa kutoa maji kutokana na kutofanyiwa matengenezo.

Amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Babati Mhandisi Felix Mollel kumuondoa katika kazi fundi wa mradi wa Maji katika kijiji cha Gidas Amos Abi.

Amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa vitendea kazi fundi huyo hakuvifanyia kazi na kusababisha baadhi ya vituo vya kuchotea maji kijijini hapo kushindwa kutoa huduma kwa wananchi.

Kadhalika Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca ametoa siku tano kwa Meneja wa RUWASA Wilayani humo kuhakikisha kasoro zilizobainika zinapatiwa utatuzi na maeneo yote yanapata maji safi na salama.

Pia amewataka Wataalamu wa maji kote nchini kutopendelea kukaa ofisini bali watembelee miradi ya maji ili kubaini changamoto na kuzitatua.