Na Mwandishi Wetu
Serikali imeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza juhudi katika usimamizi wa Rasilimali za Mawasiliano nchini, zikiwemo namba za mawasiliano ya simu, mfumo wa postikodi na rasilimali adimu za masafa.
Akizungumza kwenye viwanja vya Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa AICC wakati alipotembelea banda la maonesho la TCRA kwenye Mkutano wa Mwaka wa Wataalam wa TEHAMA uliofanyika jijini Arusha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) alisisitiza kuwa ni muhimu TCRA ikaongeza juhudi katika kazi yake nzuri ya kusimamia rasilimali hizo kwa kuzingatia kuwa Tanzania kwa sasa inajielekeza kujenga Uchumi wa Kidijitali unaotegemea sekta pana ya mawasiliano.
Pamoja na maelekezo hayo Waziri Mkuu ameipongeza TCRA kwa kazi nzuri ya kusimamia sekta ya mawasiliano nchini na kusisitiza kuwa rasilimali adimu za masafa zilindwe kwa kadri inavyopaswa. Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo baada ya kupata maelezo ya utendaji wa TCRA kutoka kwa Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta Dkt. Emmanuel Manasseh ambae alimweleza kuwa TCRA inajikita kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za mawasiliano hasa rasilimali adimu unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Akiwahutubia washiriki wa Mkutano huo Waziri Mkuu alisisitiza kuwa serikali iko thabiti katika kutekeleza azma yake ya kujenga uchumi wa Kidijitali ifikapo mwaka 2025 huku Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa nyenzo muhimu ya kufikia azma hiyo.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaimarisha uchumi wa kisasa unaotegemea TEHAMA na ninyi kama wataalam wetu mnayo nafasi ya kutufikisha kwenye uchumi huu” alisisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa Majaliwa alibainisha kuwa, serikali ipo tayari kupokea changamoto zote ambazo wataalam hao wataziainisha ili kuzipatia ufumbuzi.
"Nia ya Serikali ni kuhakikisha katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo Tanzania inatambulika kote barani Afrika na Duniani kama nchi iliyojiimarisha katika uchumi wa kidijitali" alisisitiza Waziri Mkuu. Waziri Mkuu alisisitiza kuwa mifumo yote ya TEHAMA ikiwemo ya kutoa huduma na kuwezesha utendaji wa serikali itawafikia wananchi wote walioko mijini na vijijini, ili kuhakikisha Taifa linafikia azma ya kujenga uchumi wa Kidijitali. Alibainisha kuwa katika kusambaza huduma kupitia TEHAMA serikali itahakikisha kila kona ya nchi inafikiwa na huduma za intaneti kupitia mkongo wa Taifa.
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Emmanuel Manasseh akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kuhusu shughuli za TCRA kwenye banda la maonyesho katika viwanja vya AICC, Arusha. Picha na: TCRA
Katika hatua nyingine Majaliwa alibainisha kuwa Serikali ipo katika hatua za awali za kujenga kituo kikubwa cha TEHAMA kitakachowezesha umahiri, ubunifu na utafiti katika sekta ya TEHAMA; kituo hicho kinatarajiwa kujengwa jijini Dodoma.
Kuhusu anuani za makazi Waziri Mkuu aliagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA kuhakikisha inaharakisha mchakato wa kukamilisha uwekaji wa anuani za makazi kote nchini ambazo zitaunganishwa na TEHAMA kutoa huduma kwa wananchi kote nchini.
Akizungumzia uwekezaji kwenye TEHAMA, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara kwa kushirikiana na kituo cha uwekezaji nchini kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwenye TEHAMA ili kuhakikisha lengo la kujenga uchumi wa Kidijitali linafikiwa mapema.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akiwasilisha hotuba kwa wataalam wa TEHAMA mbele ya Waziri Mkuu alibainisha kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania itakuwa imeunganishwa kwa mkongo wa taifa kwa sehemu kubwa.
“wizara imeweka mkakati wa kuhakikisha mkongo wa taifa wa mawasiliano unatandazwa maeneo yote ya nchi ili kuwezesha uzalishaji wa fursa nyingi zaidi za kiuchumi hapa nchini” alibainisha na kusisitiza Waziri Kijaji.
Kijaji alibainisha kuwa serikali imeandaa muongozo wa usajili wa wataalam wa TEHAMA nchini ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya kisera ili kuhakikisha wataalamu wote wa TEHAMA nchini wanasajiliwa kuwezesha azma ya serikali kujenga uchumi wa kidijitali ambapo lengo ni kuhakikisha kabla ya mwaka 2025 angalau wataalam 5000 wa TEHAMA wasajiliwe chini ya mpango huo.
Aidha Wizara imesisitiza nia ya serikali kuwawezesha vijana wabunifu katika TEHAMA kukuza tija na vipaji.
"Tunahitaji kuwekeza kwenye utafiti na kuwashika mkono vijana wetu wanaojishughulisha na TEHAMA" alisisitiza Waziri Kijaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Selemani Kakoso (Mb) alisisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Mawasiliano kufikisha elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA.
Mkutano huo ulioratibiwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA umehudhuriwa na wataalam wa TEHAMA zaidi ya 800 kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya Tanzania ukilenga kuyaleta pamoja mawazo ya kitaalam katika TEHAMA yatakayowezesha ukuaji wa sekta hiyo; Waziri Kijaji alitumia fursa hiyo kubainisha kuwa mkutano kama huo mwaka 2023 utafanyika Zanzibar.
****MWISHO***
0 Comments
Post a Comment