Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi(Mb)ametembelea kiwanda cha kusindika nafaka cha Ufukwe Milling Product cha Bagamoyo Pwani kinachomilikiwa na Joyce Kimaro kwa nia ya  kujifunza pia kuangalia namna Wizara ilivyoshiriki kusambaza maji ili wizara isiwe kikwazo kwa wawekezaji.

Mahundi amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na mzawa ambaye ni mwanamke ambaye amewekeza zaidi ya shilingi bilioni Nne ikiwa ni juhudi za kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu aliyetaka kila Wizara kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji.

Aidha Mahundi amefurahishwa na juhudi zilizofanywa na Joyce Kimaro za kuwekeza nchini badala ya kutegemea wageni kutoka nje.

"Wizara ya maji haitakuwa kikwazo kwa mradi mkubwa kama huu na hapa hakuna tatizo la maji",alisema Mahindi.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Joyce Kimaro ameipongeza serikali kwa kuandaa miundo mbinu rafiki kwa uwekezaji nchini zaidi akimpongeza Naibu Waziri wa maji kwa kutembelea kiwanda chake.

Kupitia ujio wa Naibu Waziri wa maji Maro ametumia fursa hiyo kuelezea changamoto ikiwemo ya ushindani sokoni na viwanda ambavyo havikidhi ubora wa unga wanaouza sambamba na kukwepa kodi.

Aidha Maro amesema kiwanda chake kinazalisha bidhaa kupitia shirika la viwango nchini(TBS)hivyo kukidhi ushindani wa kimataifa.

Amesema Kenya inazalisha kiwango kidogo cha mahindi lakini soko lake ni kubwa kutokana na usimamizi wa viwango.

Hata hivyo kutokana na uwezo mkubwa wa kiwanda hicho amesema upatikanaji wa mahindi hauridhishi kwani kwa siku kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani mia mbili sitini.

Soko kubwa la kiwanda hicho ni mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ambapo husindika unga kuanzia kilo moja hadi ishirini na tano ukiwemo unga wa lishe kwa watoto.