*MIKOA 7 KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA KUWEZESHA MNYORORO WA THAMANI WA UFUGAJI NYUKI NCHINI.*
SERIKALI imezindua Programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki ambayo itawanufaisha wananchi wa mikoa 7 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Programu hiyo ambayo inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya Shilingi bilioni 27 itatekelezwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.
Akizindua Programu hiyo leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema Serikali inafanya uchambuzi wa kitaalamu kubaini wilaya na vijiji vilivyomo ndani ya mikoa hiyo ambapo mradi huu utatekelezwa.
Amesema programu hiyo inakwenda kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya nyuki, kuwezesha maeneo ya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki, kujenga uwezo wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na taasisi zinazosimamia sekta hiyo.
Ametumia fursa hiyo kuwasihi Wakuu wa Mikoa ambayo programu hiyo inatekelezwa kutoa ushirikiano unaostahili na kuwaelimisha wananchi.
Pia ameelekeza maafisa wa nyuki wote wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kutoa mafunzo na huduma za ugani kwa wafugaji nyuki walio katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
0 Comments
Post a Comment