*MAADHIMISHI WIKI YA MAJI KITAIFA YAZINDULIWA RASMI NA MAKAMU WA RAIS*


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Mpango amezindua maadhimisho ya wiki ya Maji kitaifa akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kiutendaji, huduma ya majisafi na salama pamoja na usafi wa mazingira mijini na vijijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na kusababisha mageuzi makubwa ya kisekta.


Akitahadharisha kuwa ni muhimu kutunza mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji kwa kuwa ndio msingi mkuu wa huduma bora ya maji na yenye uhakika.


Vilevile, Dkt. Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa kuing'arisha Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa na nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini.


Awali, Dkt. Mpango aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji Orkesumet wilayani Simanjiro  wenye thamani ya Shilingi bilioni 41.5 ambao utekelezeji wake umefikia asilimia 99 chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA)  na kutoa pongezi kwa kazi nzuri iliyofanywa na mamlka hiyo.


Aidha, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kuwa  kwa sasa hakuna changamoto ya utekelezaji wa miradi na kuwataka wataalam wa Sekta ya Maji kuongeza ufanisi katika kusimamia, kuendesha na matengenezo ya miradi hiyo kwa dhumuni la kutoa huduma kwa miaka mingi ijayo.


Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanaadhimishwa nchini kila mwaka tarehe 16-22 Machi, ambapo kilele cha maadhimisho hayo mwaka huu yatafanyika Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.