WATU 4 WENYE ULEMAVU KUTOKA FAMILIA MOJA KAGERA  WATUMIA MITI YA MIHOGO KUTEMBELEA WAILILIA SERIKALI


Na Lydia Lugakila, Kagera


Watu wanne wa familia moja katika kijiji cha Bumilo kata ya Kibanga wilayani Muleba Mkoani Kagera wameeleza kupitia magumu baada ya kukosa mahitaji yao kutokana na hali waliyonayo ya ulemavu huku wakiiomba serikali kuwasaidia nyenzo za kutembelea kutokana na kutumia fimbo ya mti wa muhogo ikiwa ni pamoja na kutokuwa na uhakika wa kupata chakula kutokana na hali yao kiuchumi.

 

Wakizungumza na mtandao huu wanafamilia hao akiwemo  Bi, Geraidina Deogratias mwenye umri wa miaka  (58) mama wa familia, Wilson Deogratias Kaka wa familia (35) pamoja na Asted Deogratias (19) wamesema kuwa wanapitia hali ngumu ya maisha kutokana na hali yao kiuchumi, ukosefu wa nyenzo za kutembelea jambo linalowalazimu kutumia nyenzo zisizo maalum ikiwemo fimbo ya mti wa muhogo ambayo haiendani na hali waliyonayo.


Kufuatia hali hiyo kaka wa familia Wilson ameiomba jamii kuwa na huruma huku akieleza namna alivyorudishwa nyuma kimaendeleo katika juhudi za kuikomboa familia hiyo baada ya kibanda alichoanzisha kuporwa na wezi.


"Licha  ya hali yangu niliyonayo bado napitia changamoto zaidi kwani nilibahatika kupata mtaji wa shilingi laki 8 nilizokopa nikaanzisha kibanda cha bidhaa za mahitaji ya nyumbani wezi walinikomba kila kitu hadi sasa sijapata wala kuwapata watu waliotenda tukio hili hivyo naomba serikali, mashirika na watu binafsi watuangalia kwa jicho la huruma kwa kutupatia nyenzo, mitaji, mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze kuzitunza familia zetu" alisema Wilson.


Akizungumzia hali hiyo Baba wa familia mzee Deogratias Paul mwenye umri wa miaka 80 amesema familia hiyo yenye kijana mwenye  watoto 3 imeamua kujibana katika nyumba moja na kufanya familia hiyo kuwa na jumla ya watu 9 huku mzee huyo akitegemewa zaidi katika kuitafutia mkate familia yake.


Naye Mtoto Asted Deogratias amesema kuwa ameamua kuacha shule akiwa darasa la sita kutokana na umbali mrefu wa kuifuata  huduma hiyo pamoja na uwezo mdogo wa familia hiyo huku akiiomba serikali kumwezesha walau ajifunze kazi za mikono kuikomboa familia hiyo ili isije tumbukia katika wimbi la omba omba.


Aidha kwa upande wake Bi Geraidina mama wa familia ameongeza kuwa alipata ulemavu wa miguu yote miwili akiwa na umri wa mwaka mmoja huku watoto wake watatu wakipata ulemavu wa miguu wakiwa wakubwa ambapo ameiomba kujenga utamaduni wa serikali kuwashirikisha watu wenye ulemavu, kupatia elimu ya kijitambua, kupatia mikopo na  kuwaboreshea miundo mbinu kwani iliyopo si rafiki kwao.