WATUMIAJI ALAMA ZA UBORA TBS KANDA NYANDA ZA JUU WAKABIDHIWA LESENI NA VYETI.

Watumiaji wa alama za ubora zaidi ya 50 kutoka mikoa sita ya Iringa,Njombe,Mbeya Songwe,Rukwa na Katavi wamekabidhiwa vyeti na leseni za utumiaji alama za ubora na Shirika la Udhibiti Viwango vya Ubora TBS.

Akikabidhi leseni na vyeti kwa watumiaji hao Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Mbeya Mwajabu Nyamkomola amesema watumiaji wanapaswa kuendelea kusimamia ubora wa bidhaa zao kwa nia ya kuboresha huduma kwa walaji.

Amesema watumiaji wa alama za ubora wa TBS waliokabidhiwa leseni wamepewa heshima hiyo na Shirika la kudhibiti Viwango vya Ubora TBS baada ya kutathmini ubora wa bidhaa zao.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la kudhibiti Viwango vya Ubora TBS Lazaro Msasalaga amesema TBS itaendelea kusimamia na kudhibiti Viwango vya Ubora ili bidhaa zinazozalishwa ziwafikie walaji kwa viwango vinavyostahili.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBS Kanda Nyanda za Juu Ernest Simon amesema jumla ya watumiaji alama za ubora 56 kutoka mikoa sita wamekabidhiwa vyeti na leseni baada ya kukagua ubora wa bidhaa zao.