Watoa Huduma za Kiposta
Waaswa kuzingatia Sheria
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaasa watoa
huduma za Posta nchini kuzingatia sheria, kanuni na miongozo wanapowahudumia
wananchi kwa kusafirisha vifurushi na vipeto vyao kwenda maeneo mbalimbali.
Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta ya mwaka 2010 imepewa jukumu la kusimamia sekta ya Mawasiliano na Posta.
Akizungumza kwenye Mkutano na wadau wa usafirishaji
vifurushi na vipeto wapatao 70 uliofanyika jijini Dar es salaam, Afisa
Mwandamizi wa Kitengo cha Huduma za Posta wa Mamlaka hiyo Joseph Zebedayo
alisisitiza kuwa ni muhimu watoa huduma za kiposta kuhakikisha wanazingatia
sheria, kanuni na masharti ya leseni ili kuwapa wananchi huduma zenye viwango
na vinavyotoa uhakika wa huduma.
“Tumekutana na wadau hawa ili kuwaelimisha kuhusu
huduma wanazotoa na lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri za
usafirishaji wa vifurushi na vipeto ukizingatia huduma hizi ni muhimu katika
kuleta Maendeleo yetu,” alibainisha.
Mamlaka hiyo imekutana na wadau hao pembezoni mwa
kampeni ya Elimu kwa umma inayotekelezwa kote nchini iitwayo “Tuma Chap kwa
Usalama” ikilenga kuwahamasisha watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na
vipeto nchini kuhakikisha wanasajili huduma zao kwa kupata leseni ya TCRA na
wananchi kuhakikisha wakati wote wanapotumia huduma za usafirishaji vifurushi
na vipeto wanatumia watoa huduma waliosajiliwa.
Pembezoni mwa Mkutano huo Afisa Mawasiliano Mwandamizi
Mkuu Semu Mwakyanjala alibainisha kuwa TCRA inaendesha Elimu kwa umma iitwayo
Tuma Chap, Kwa Usalama inayolenga kuwapa wananchi Elimu ya usafirishaji vipeto
na vifurushi ili kuongeza tija ya mchango wa sekta ya posta kwenye uchumi.
“Mamlaka tunawakumbusha wananchi kuzingatia kutuma
vifurushi na vipeto kwa mtoa huduma aliesajiliwa na watoa huduma kupata leseni
ya TCRA ili kutoa huduma za kusafirisha Bidhaa za kiposta yaani vipeto na
vifurushi, pia wale ambao leseni za kutoa huduma zimefikia ukomo tunawaasa
wahuishe leseni hizo, kwani kutoa huduma za kiposta bila leseni ni kwenda
kinyume na sheria,” alibainisha.
Mamlaka hiyo aidha ilionya kuwa watoa huduma
wanaosafirisha vipeto na vifurushi wasiosajiliwa watambue kwamba kufanya huduma
bila usajili ni kutenda kinyume na sheria. Huku ikiwataka kuzingatia sheria
bila kushurutishwa.
“Sheria ya Mawasiliano iko wazi; ikiwa unahitaji kutoa
huduma zozote za Mawasiliano katika nchi yetu sharti uwe na leseni, hivyo
niwakumbushe wenzetu (watoa huduma) kuhakikisha wanakata leseni ndipo watoa
hizi huduma,” alibainisha Afisa Mawasiliano.
Ushindani katika sekta ya posta kwa mara ya kwanza
uliruhusiwa Tanzania mwaka 1989 kwa kutumia Sheria Posta na Simu ya wakati huo
ambayo iliruhusu posta binafsi ya kwanza kusajiliwa na kuanza kutoa huduma.
Mageuzi ya sekta ya mawasiliano yalianza rasmi 1994 ambayo iliweka ushindani
wenye masharti yaliyowekwa na Mdhibiti wa Sekta. Kwenye miaka ya mwanzo ya 2000
makampuni binafsi mengi ya usafirishaji nyaraka, vipeto na vifurushi
yalisajiliwa yakiwemo mabasi ya abiria. Hadi sasa kunawatoa huduma za Kiposta
na Usafirishaji wa Vifurushi na Vipeto wapatao 96, likiwemo Shirika la Posta.
0 Comments
Post a Comment