Mifumo 14 Yaunganishwa NeST


Mfumo mpya wa ununuzi “National e-Procurement System of Tanzania” (NeST) umeunganishwa na mifumo 14 ili kuondoa usumbufu kwa wazabuni kuambatanisha nyaraka mbalimbali wanapoomba zabuni taasisi za umma.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imetaja mifumo iliyounganishwa na NeST kuwa ni BRELA -ORS, TRA-TIN, MUSE, GePG, TAUSI, HCMIS, CRB, ERB, ERMS, PlanRep, PSTPB,OSHA, TIRA na AQRB


Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mifumo mingine ambayo ipo kwenye hatua za kuunganishwa ni mifumo ya kibenki. Aidha, PPRA inaendelea na juhudi za kuunganisha mifumo inayohifadhi na kuchakata taarifa mbalimbali za wafanyabiashara/wazabuni waliosajili biashara zao Tanzania Visiwani (Zanzibar).


Taarifa hiyo imeeleza faida za mfumo wa NeST kuwa ni pamoja na kusajili taarifa mara moja na kuzitumia kwa zabuni zote zinazoombwa na hivyo kupunguza muda unaotumika katika kuomba zabuni.


“Mzabuni hatakuwa na haja ya kuweka viambatisho vya vyeti au uthibitisho wa usajili kutoka kwenye Taasisi mbalimbali. Mzabuni atatakiwa kuweka namba ya uthibitisho na taarifa nyingine zitapatikana kutoka kwenye mifumo iliyounganishwa,” imefafanua taarifa hiyo.


Aidha, Mzabuni anaweza kujisajili au kuomba zabuni popote alipo kwa kutumia simu yake ya mkononi (Mobile Application). Pia kufuatilia na kupata taarifa ya hatua za zabuni mzabuni aliyoomba (tender progress tracking).