Na Dixon Busagaga ,Ngorongoro.

MWANAMKE mmoja aliyepoteza Jicho,Masikio pamoja na Viganja vya mikono yake miwili baada ya kushambuliwa na fisi wakati akinusuru mifugo yake isiliwe katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ameiomba Serikali kumpatia msaada ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kutoka katia eneo hilo.

Rose Kapande (50) Mkazi waa Kijiji cha Esapai kata ya Nainokanoka wilaya ya Ngorongoro ,mkoani Arusha anasema alifikwa na mkasa huo mwaka 2018 ,fisi huyo  anayetajwa kuwa na kichaa cha Mbwa pia akifanikiwa kuua Ng;ombe wanne .

Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro linatajwa kama eneo la Uhifadhi Mseto ,masuala matatu yakifanyika kwa maana ya Uhifadhi ,uendelezaji wa jamii inayoishi katika eneo hili pamoja na utalii wakiruhusiwa binadamu jamii ya wafugaji ,Mifugo ,Ng’ombe,Mbuzi na Kondoo kuishi pamoja na Wanyamapori.

Hata hivyo utaratibu huo baadhi ya nyaraka zinaeleza kuwa ulikuwa ni sehemu ya majaribio kuona kama inawezekana ukilenga kutizama uwiano wa mambo matatu kwa maana ya Uhifadhi ,maendeleo ya jamii na utalii.

Changamoto iliyopo sasa kwa wakati huu ni idadi ya watu kuongezeka kutoka 8000 hadi kufikia 100,000 mara 10 zaidi,wakati hiofadhi hii ikianzishwa,mifugo ikiongezeka hadi kufikia Milioni moja kutoka 260,000.

Ongezeko la idadi ya watu na Wanyama limechangia kupungua kwa eneo la malisho pamoja na muingiliano wa wanyamapori na wananchi ambao pia umechangia uwepo wa muingiliano wa magonjwa yanayotoka kwa mifugo,wanyamapori na binadamu.

Matukio mbalimbali ya vifo vitokanavyo na wanyapori kwa binadamu na wakati mwingine kusababisha ulemavu yanatajwa kuchangiwa na ongezeko hili la Binadamu na mifugo .

Rose Kapande mama wa watoto tisa aliyekuwa akiishi peke yake kwenye Boma baada ya kutalikiana na mumewe ni mmoja wa waathirika wa matukio ya kuvamiwa na kisha kushambuliwa na Wanyamapori ,akipoteza viganja vya mikono ,Jicho moja ,Masikio pamoja na fuvu la kichwa .

Anaeleza kuwa wakati wa tukio, majira ya saa nane usiku alikuwa amelala ndani peke yake  siku hiyo na baadae alisikia kitu kinagongagonga kwenye zizi la Ng’ombe ndipo alipoamua kutoka nje kuona ni kitu gani .

Wakati anafungua mlango alimuona fisi akipambana na mifugo yake upande wa Ndama ndipo kwa ujasiri alianza kumfukuza Fisi yule asile mifugo ,wakati akimfukuza ghafla Fisi yule alimgeukia na kuanza kumshambulia sehemu za mikono, kichwa na sehemu ya uso ambapo  aliliwa jicho moja la upande wa kulia.

“Wakati natoka nje nikamwona fisi,  nikawa namtishia ili aondoke, yule fisi akanigeukia akaanza kupambana na mimi, alinishika na kuanza kunijeruhi kwa kunichanachana sehemu ya fuvu la kichwa na sehemu ya uso upande wa kulia ambapo alinitoa hadi jicho, kwa hiyo upande mmoja wote uliharibika na mikono yote aliitafuna,”

“Baada ya kunijeruhi alirudi tena kwenye boma la Ng’ombe na kuwajeruhi tena mifugo iliyokuwepo ndani, baada ya kuniachia nikiwa na majeraha makali, nilipiga ukunga, bahati nzuri majirani zangu  walikuja kunisaidia ambapo walinichukua na kunipeleka hospitali ya KKKT, Karatu, baadaye nilipelekwa Hospitali ya Mount Meru ambayo iko Arusha na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC kwa matibabu makubwa zaidi,”alisema Rose .

Rose anasema kwa sasa hali ya maisha yake ni magumu kwa kuwa hana mikono tena na upande mmoja wa kichwa na sehemu ya uso vyote viliharibiwa na fisi na kwamba hawezi kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato.

“Mimi ni mlemavu, sina mikono na upande wangu mmoja wa kichwa na uso ni mbovu, nipo tu hapa nasaidiwa na wasamaria wema maana watoto wangu wote walishaolewa, kwa hiyo chakula nalishwa kama mtoto mdogo, nguo navalishwa yaani sijiwezi chochote hapa nilipo,”alieleza Rose huku akisaidiwa kunyweshwa uji.

“Naishukuru serikali nimepona mpaka  kwa namna ambavyo walinipigania kuokoa maisha yangu, nimebaki mlemavu na hali yangu ya Maisha ni ngumu, mpoaka sasa kutokana na Maisha niliyopitia naishi kwa hofu hapa niluipo kutokana na Wanyama wakali walipo katika hifadhi hii,”

Rose anasema kwa kuwa amekuwa akiishi kwa hofu ameiomba serikali imsaidie aondoke katika eneo la hifadhi Ngorongoro imtafutie sehemu nyingine ya kwenda kuishi kama ambavyo watu wanavyohamishwa kwa sasa.

“Mimi niliomba kuondoka hata kabla ya huu hili zoezi la kuwaondoa watu halijaanza, naomba serikali inisaidie niende kuishi  sehemu salama zaidi, nitafurahi sana maana najua nitakwenda kuishi sehemu salama nikitoka huku hifadhini maana maisha yangu kwasasa yamekuwa na hofu kubwa sana tangu nijeruhiwe,” alieleza Rose

Akizingumza kwa kwa lugha ya kabila la Maasai na kusaidiwa tafsiri na Jirani yake aliyefahamika kwa jina la Samweli ,Rose ameiomba serikali impatie  msaada kwani hapo alipo ni mlemavu na hakuna chochote ambacho anaweza kufanya cha kumpa rizki.

“Mimi ni miongoni mwa watu ambao nilienda kutembelea Msomera maisha ya kule nayaona ni mazuri yatanifaa zaidi na nitakuwa nimesaidiwa sana na serikali, naiomba serikali iharakishe kukamilisha mpango wa sisi kwenda kule Msomera maana naona kama vile nacheleweshwa kuondoka maana tunaelendelea kuishi katika mazingira hatari huku hifadhini na wanyama,”

Samweli na Petro Kashuu ni majirani wa mama huyu hapa wanaeleza namna ambavyo walishuhudia tukio hilo wakisema maisha ya watu katika eneo hilo yapo hatarini kutokana na uwepo wa Wanyama hatari kama Simba,fisi ,Mbwa mwitu ,Nyati na Tembo na watu wamekuwa wakiishi kwa hofu.

“Huyu mama wakati alipojeruhiwa na fisi tulikuwepo, na hili eneo limekuwa na fisi wengi, tumekuwa tukiteswa na Wanyama hapa kijijini, maisha ya huku ni hatari kwasababu wanyama wamekuwa wakitujeruhi licha ya kwamba huku watu wamezoea kuishi na Wanyama.

“Yule Fisi baada ya kumshambulia huyu mama alienda kwenye zizi na kushambulia Ng’ombe wanne ,mmoja alikufa siku hiyo hiyo akachinjwa watu wakala,baada ya siku mbili wale Ng’ombe wengine walikufa pia “ alisema Kashuu .

Kashuu alisema yule Fisi walifanikiwa kumuua na baadae alifanyiwa vipimo kwenye kituo cha utafiti na kubainika kw amba alikuwa na Kichaa cha Mbwa .” Inasemekana yule fisi kabla ya kuja kuvamia kwa huyu mama aling’atwa na Mbwa akapata kichaa cha Mbwa “.

Naibu Kamishna  Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Elibariki Bajuta amethibitisha kutokea kwa matukio ya namna hiyo akieleza baada ya tukio  la Rose Kapande amesema serikali ilifanya jitihada za haraka kuokoa maisha ya mwanamke huyo kwa kuhakikisha anapata matibabu yanayostahili.

“Ni kweli tunafahamu tukio hili la huyu mama kujeruhiwa na fisi na viungo vyake kuliwa na fisi, huyu mama alikwenda kuokoa mifugo yake baada ya kusikia fisi ameingia kwenye boma la ng’ombe hivyo wakati anapambana kuokoa mifugo yake alivamiwa na fisi,”

“Fisi walitafuna viganja vyake vya  mikono  na sehemu kubwa ya uso na  upande wa kulia wa kichwa chake na kumuathiri upande wa kulia wa fuvu na sehemu ya mdomo,”

“Mamlaka kwa kuwa tuna kituo cha ulinzi na timu za uokoaji baada ya kupata taarifa hizi vijana wetu kwa kushirikiana na majirani tumlimsaidia kuhakikiasha anapata huduma stahiki,”

Aidha alisema matukio ya watu kuathiriwa na kuvamiwa na wanyama wakali katika hifadhi hiyo ni mengi  na kwamba  yapo matukio ya watu kuumizwa  na wanyama kama vile  chui, fisi, simba na tembo .

“Sisi kama Mamlaka tunaendelea kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari  lakini mnyama ni mnyama tu hazoeleki, tunafurahi mama huyu kwa sasa anataka kuhama hifadhini kwenda sehemu anayotaka na suala hili la watu kutakiwa kuhama kwa hiari ni kwa ajili ya usalama wa maisha yao na uhifadhi.

Mwisho