JUMLA YA WAZABUNI 4,350 WAMEJISAJILI KWENYE MFUMO WA NeST.


Na Mwandishi Wetu,  Dodoma.


Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA yawasisitiza Wafanya biashara na Wazabuni wote nchini Kuendelea kujisajili katika Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya mtandao NeST ili kuongeza ushindani na kupanua wigo Mpana katika kuboresha uendeshaji wa Michakato ya ugawaji wa zabuni za umma.


Akizungumza hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA Bw. Eliakim Maswi amesema kuwa, Idadi ya Wazabuni wanaojisajili kwenye Mfumo inazidi kuongezeka siku hadi siku jambo linalotoa taswira Chanya juu ya muitikio na mapokeo ya Wananchi katika ujio wa Mfumo huo mpya wa NeST katika sekta ya Ununuzi wa Umma.


“Tunashkuru kupitia juhudi za Serikali yetu Kuona idadi ya Wazabuni wanaojisajili ndani ya Mfumo inaongezeka siku hadi siku suala ambalo hata sisi kama Mamlaka tunalitazama kwenye mtazamo Chanya, Mpaka sasa Jumla ya Wazabuni 4,350 tayari wameshajisajili kwenye Mfumo” Alisema Maswi.


Sambamba na suala hilo, Maswi amewataka Wazabuni Pamoja na Taasisi za Umma kuendelea kushiriki mafunzo yanayoendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini ambayo yanalenga kutoa muongozo wa namna ya matumizi sahihi ya Mfumo huo wa NeST kwa Taasisi za Umma sambamba na Wazabuni wake.


“Utaratibu wetu wa utoaji Mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo bado unaendelea, Kwahivyo niwasihi Wazabuni Pamoja na Taasisi mbalimbali za Umma kuweza kushiriki mafunzo hayo kwa mujibu wa ratiba zinazopangwa” Aliongezea


Aidha amesema kuwa, Sambamba na Utoaji wa mafunzo hayo wanahakikisha  kila Taasisi inayopatiwa mafunzo inasajiliwa ndani ya Mfumo mpya wa NeST ili mapema kuanza kutumia Mfumo huo bila kuwa na urasimu wa aina yoyote.


“Kila Taasisi tunayoipatia mafunzo ya Mfumo mpya tunahakikisha tunaisajili pia kwenye mfumo ili ikibidi waanze kutumia mfumo huu haraka” Alisema


Ifikapo tarehe 30 Septemba Taasisi zote za Umma zinatakiwa ziwe tayari zimeshajisajili kwenye Mfumo kwani Mpaka tarehe 1 Oktoba hakutakuwa na Taasisi yoyote ya Umma itakayoweza kufanya michakato ya Ununuzi nje ya mfumo wa NeST.