Meneja wa TCRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mhandisi Asajili John akimpa zawadi ya mfuko wenye nembo ya TCRA Naibu Waziri wa Uchukuzi na ujenzi Mhe. Engineer Godfrey Kasekenya muda mfupi baada ya kuzuru banda la TCRA kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya yalikofanyika maonesho ya kilimo kitaifa.

Afisa wa TCRA Bi. Jasmine Kiyungi akimhudumia mtoa huduma za mawasiliano kwenye banda la TCRA katika viwanja vya maonesho ya Nanenane kitaifa yaliyofanyika jijini Mbeya


TCRA Yajidhatiti utoaji Elimu kwa Wakulima, NaneNane


Na Mwandishi Wetu


Wakati wakulima wakikusanyika kusherehekea sikukuu ya NaneNane, inayojulikana pia kama Siku ya Wakulima, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imechukua jukumu la kutoa elimu kwa umma ili kuimarisha matumizi salama ya huduma za mawasiliano na matumizi sahihi ya mtandao.


Mamlaka hiyo imeshiriki kikamilifu kutoa Elimu kwenye Maonesho yanayoadhimishwa Kitaifa mkoa wa Mbeya kwenye viwanja wa John Mwakangale vilivyopo Uyole na Maonesho yanayofanyika katika viwanja vya Kizimbani Dole Wilaya ya Magharibi “A” Unguja, Zanzibar. 


Akizungumza katika Siku ya Wakulima (NaneNane) kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja wa TCRA wa Kanda ya Nyanda za Juu-Kusini Mhandisi Asajile John, na Kaimu Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma, Bw. Rolf Kibaja, walisisitiza umuhimu wa watumiaji wa huduma za mawasiliano hasa mawasiliano ya simu nchini kushiriki katika kupambana na utapeli unaotendwa kupitia mawasiliano ya simu. 


"Tungependa kuwakumbusha wakulima wote kwamba wanaweza kuchukua jukumu la kuhakikisha usalama wao mtandaoni kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyosimamia sheria kwa kutoa taarifa. Ikiwa unapokea ujumbe wa SMS ya ulaghai, usifute ujumbe huo. Badala yake, ripoti namba za matapeli kwenda namba 15040. Jeshi la Polisi litachukua hatua stahiki na haki itatendeka," aliomba Mhandisi Asajile John.


Alibainisha kuwa, mara baadhi ya taarifa kutolewa namba zinazojihusisha na utapeli kwa njia ya simu hufungiwa kutoa na kupokea huduma mara moja wakati hatua nyingine za kiudhibiti huchukuliwa zikiwemo kuwatafuta wahalifu, jukumu ambalo hutekelezwa na jeshi la Polisi. 


"Kuwa makini unapopokea ujumbe uliotumwa kwenye simu yako na mtu mwingine hasa usiemfahamu ambao unakushawishi kutekeleza maelekezo yanayohusu miamala ya kifedha. Tunakushauri kufuta ujumbe kama huo mara moja ili kujilinda dhidi ya watu wenye nia ovu," alitoa ushauri Bw. Rolf Kibaja.


Kuhusu upatikanaji wa leseni za kutoa huduma za mawasiliano, Kibaja alisisitiza kuwa, TCRA sasa imeboresha namna mtu anavyoweza kupata leseni hizo.


“TCRA imeanzisha Tanzanite Portal, mfumo bora wa kupata leseni mtandaoni. Hakuna haja tena ya kusafiri hadi ofisi za TCRA. Kuomba au kuhuisha leseni yako sasa unaweza kufanya zoezi hilo kwa urahisi kupitia Tanzanite Portal, tembelea tovuti yetu na wasilisha maombi yako ya leseni," alithibitisha Bw. Rolf Kibaja na kuongeza kuwa, Mamlaka hiyo imeweka mfumo huo ili kupunguza muda ambao mtu anaweza kupata leseni ili kutoa huduma kwa wananchi, alibainisha kuwa mfumo huo sasa unaruhusu na kupokea maombi ya leseni kubwa na ndogo za kutoa huduma za mawasiliano nchini. 


Katika juhudi zao za kushughulikia haraka masuala ya watumiaji wa huduma za mawasiliano wakiwemo wakulima, TCRA ilishirikiana kwa karibu na Kampuni za Simu za Mkononi ili kuhakikisha ufumbuzi wa malalamiko kwa ufanisi. Katika banda, malalamiko yote yaliyopokelewa yaliandikishwa, na kampuni za simu zilifanya kazi kwa karibu na maafisa wa Mamlaka kutafuta ufumbuzi wa masuala ya watumiaji wa huduma za mawasiliano. Kampuni zilizokuwepo katika banda la TCRA Mbeya ni Vodacom, Tigo, Halotel, na Airtel.


Elimu kwa wakazi wa Zanzibar

Ili kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaendelea kunufaika na huduma za mawasiliano na wanakuwa salama wakati wanapotumia huduma hizo TCRA ilishiriki kikamilifu katika utoaji Elimu kwa umma katika viwanja vya Dole, ambapo wakaazi na wakulima wa Zanzibar walitembelea banda la TCRA na kupokea elimu kamili. Afisa Mkuu wa Mawasiliano Bw. Semu Mwakyanjala alielezea furaha yake kwa idadi ya wakaazi wa Zanzibar waliohudhuria banda hilo.


"Idadi ya wakaazi wa Zanzibar waliohudhuria banda la TCRA imefurahisha na kutia moyo kwamba wananchi wetu wanahitaji Elimu haswa. Mamlaka imewapa elimu ya ufahamu kwa kadri inavyostahili," alisema Bw. Semu Mwakyanjala.


Banda hilo liliwapa wakulima ufahamu muhimu juu ya jukumu na majukumu ya TCRA katika sekta ya mawasiliano. Elimu iliyotolewa ni pamoja na uelewa kuhusu majukumu ya kazi za TCRA. Pia, Elimu ya kujilinda mtandaoni ilitolewa.


“Tumewaeleza Ndugu zetu waliotutembelea hapa kwamba wawe makini wanapotumia huduma za mawasiliano ya simu, wasitoe ushirikiano kwa mtu yeyote anaehitaji taarifa zao binafsi na wasifungue viunganisho vya mtandaoni bila kujiridhisha chanzo cha link hizo,” alisema.


Alibainisha kuwa matapeli wamebuni mbinu ya kuingilia mawasiliano ya watumiaji kwa kutuma link ambazo mtumiaji anapoifungua na kutoa ushirikiano kwa maelekezo yao basi huwa rahisi mawasiliano yake kuingiliwa kiurahisi.


Wakulima waliotembelea Mamlaka hiyo kwenye viwanja vya maonesho ya kilimo ya kitaifa na Zanzibar walitoa pongezi kwa TCRA kwa kazi nzuri ya kuwaelimisha wakulima kuhusu usalama mtandaoni. Alinanuswe Mwakanyamale, mkulima wa ndizi kutoka wilaya ya Nditu Rungwe, alisema, "Nimetembelea banda la TCRA na nimejifunza mengi. Sisi wakulima daima tumekuwa tukidanganywa na wadanganyifu wa mtandaoni, haswa wakati wa mavuno, tunashukuru TCRA kwa kuja katika tukio letu na kutupatia elimu hii muhimu."


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya nae mara baada ya kutembelea banda la TCRA Mbeya alibainisha kufurahishwa na namna TCRA ilivyojidhatiti kuwaelimisha wananchi ili kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wanapotumia huduma za mawasiliano. 


***