Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt Leonada Mwagike akitoa Muhtasari wa Ripoti ya Utendaji kazi kwa mwaka 2022/2023 mbele ya Naibu waziri wa Fedha Mh. Hamad Chande (Mb). wakati wa tukio la kukabidhi ripoti hiyo.
PPRA yaokoa zaidi ya Bilioni 2 katika Ununuzi wa Umma.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 2.6 za Kitanzania kwa kufanikiwa kuzuia malipo yaliyokiuka utekelezaji wa mkataba katika ununuzi wa umma pamoja na kusudio la baadhi ya wazabuni kukwepa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) .
Yameelezwa hayo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike alipokuwa akikabidhi Ripoti ya ukaguzi katika Ununuzi Serikalini kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Kwa Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), hafla iliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Dkt. Mwagike alieleza PPRA ilibaini hayo wakati wa utekelezaji wa majukumu yake katika ukaguzi wa Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na Wizara ambapo jumla ya Taasisi mia themanini zilikaguliwa. Ukaguzi huo ulijikita katika kuangalia taratibu za ununuzi na utekelezaji wa mikataba.
Dkt. Mwagike alieleza kutokana na ukaguzi uliofanyika PPRA ilibaini baadhi ya wakandarasi walikwepa kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika kazi walizozifanya Serikalini hali hiyo ilipelekea PPRA kuelekeza wasilisho la stakabadhi hizo kabla ya zoezi la ukaguzi kuisha. Jumla ya stakabadhi zenye thamani ya TZS milioni 290 ziliwasilishwa.
“Fedha zote hizi zilizopatikana kutokana na malipo ya kodi ya ongezeko la thamani zimerudishwa Serikalini” Alisema.
Alieleza kuwa fedha nyingine zilizookolewa zilitokana na malipo yaliyolipwa kwa mtoa huduma ambayo hayakuwa sahihi, malipo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 233 yalirejeshwa Serikalini.
Aidha malipo yenye thamani ya shilingi bilioni .
1.7yaliokolewa kutokana na kusitisha malipo ya huduma iliyotolewa chini ya kiwango kwa moja ya Taasisi ya Umma hali iliyopelekea PPRA kuelekeza taasisi husika kukatisha mkataba na mzabuni.
Dkt. Mwagike alieleza licha ya fedha hizo kurudishwa Serikalini kwa ajili ya matumizi mengine ya maendeleo pia PPRA imemfungia mzabuni mmoja ambaye alihusika moja kwa moja na makosa ya kutoa huduma chini ya kiwango na kutaka kuisababishia Serikali hasara. Mzabuni huyo hataruhusiwa kutoa huduma yoyote Serikalini.
Katika ripoti hiyo Mamlaka ilipendekeza hatua mbalimbali kuchukuliwa na Serikali kwa Taasisi ambazo zimeisababishia Serikali hasara.
“Mamlaka inatoa mapendekezo mbalimbali kwa Taasisi Nunuzi husika ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika na mchakato wa ununuzi iliyosabaisha hasara kwa Serikali” Dkt. Mwagike
Hii ni ripoti ya 17 kuwasilishwa kutokana na tathmini ya mwaka ya utendaji kwa taasisi za umma ikiweka tamati ya ripoti zilizowasilishwa mbele ya Waziri wa Fedha ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 ripoti hiyo rasmi itakuwa iikiwasilishwa moja kwa moja kwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 Comments
Post a Comment