Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.Prosper Mgaya akizungumza na wafanyakazi wa VETA (hawapo pichani) kwa ajili ya kuanza kazi katika Mamlaka hiyo , jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.Prosper Mgaya akizungumza na wafanyakazi wa VETA kwa ajili ya kuanza kazi katika Mamlaka hiyo , jijini Dodoma.Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.Prosper Mgaya (Kushoto) akipokea nyaraka kutoka kwa aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo CPA.Anthony Kasore kama ishara ya kumkabidhi Ofisi, alipowasili katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dodoma, leo tarehe 6 Novemba, 2023.
Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imemteua Dkt. Prosper Lutangilo Mgaya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Dkt. Mgaya anachukua nafasi ya Dkt. Pancras Bujulu ambaye alistaafu utumishi wa umma mwezi Machi, 2022 na nafasi hiyo kukaimiwa na CPA Anthony Kasore ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha wa VETA. Uteuzi wa Dkt. Mgaya ni kuanzia tarehe 1 Novemba, 2023. Kabla ya Uteuzi huo Mgaya, alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi.
Akizungumza na wafanyakazi wa VETA Makao Makuu katika ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dodoma alipowasili rasmi leo tarehe 6 Novemba, 2023, Dkt. Mgaya amesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutoa ujuzi kwa Watanzania kupitia vyuo vya VETA nchini yanafikiwa.
Amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha vyuo vya VETA vinakuwa karibu zaidi na wananchi ili watanzania wa ngazi zote waweze kujipatia ujuzi hivyo VETA ina jukumu la kuweka mipango na mikakati thabiti katika kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali.
“VETA inatoa mafunzo yanayogusa asilimia kubwa ya Watanzania na mafunzo hayo ndiyo yanayotegemewa kubadilisha maisha ya wananchi wengi kiuchumi…Ni wajibu wetu kufanikisha utoaji wa mafunzo hayo kwa ubora na umahiri,”amesema
Dkt. Mgaya amewataka wafanyakazi wa VETA kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuwasihi kumpatia ushirikiano katika kufanikisha malengo ya Mamlaka hiyo na mategemeo ya Serikali.
Amewasihi wafanyakazi kufanya kazi kwa ushirikiano na kutambua umuhimu wa mchango wa kila mmoja katika kufikia malengo ya taasisi.
''Kila mmoja ana sifa zake ambazo Mungu amemkirimia kuweza kuisaidia VETA kusonga mbele. Ni juu ya viongozi kuangalia nani mzuri kwenye eneo gani na asaidie wapi?''amesema.
Ameongeza kuwa yeye kama kiongozi aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, hana ufumbuzi wa kila changamoto aliyoikuta, bali ushirikiano wa pamoja miongoni mwa wafanyakazi ndio utakaowezesha kutatua kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto na kusonga mbele.
Awali Mkurugenzi wa Fedha wa VETA aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, CPA Anthony Kasore amempongeza Dkt. Mgaya kwa kuteuliwa na kueleza imani yake kwa Dkt. Mgaya katika kufanya mageuzi ndani ya VETA hasa kwa kuzingatia kuwa amebobea na ana uzoefu wa kutosha kwenye eneo la ufundi.
CPA Kasore amewasihi watumishi wa VETA kumuunga mkono Mkurugenzi Mkuu huyo mpya kwa kutimiza wajibu wao kwa uaminifu na ufanisi ili kuleta mafanikio kwenye Taasisi hiyo.
Akimkaribisha na kutoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa VETA, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi VETA Makao Makuu, Ndg. Christopher Msigwa amempongeza Dkt. Mgaya kwa kuteuliwa kuiongoza VETA na kumtakia utendaji kazi bora katika nafasi yake.
Dkt. Mgaya ni Mhandisi mbobevu katika masuala ya Rasilimali Maji (Water Resources
Engineering). Amekuwa kwenye utumishi wa umma akiwa mhadhiri na akishika nafasi
mbalimbali za uongozi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha
Taifa cha Usafirishaji (NIT). Vilevile, Dkt Mgaya ni Mwenyekiti wa Bodi ya Sayansi na
Teknolojia Shirikishi (Science and Allied Technologies) ya Baraza la Elimu ya Ufundi na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET). Pia ameshika nafasi mbalimbali za usimamizi,
utafiti na ushauri elekezi kwenye taasisi na miradi mbalimbali.
0 Comments
Post a Comment