Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Naibu Spika Dkt Tulia Ackson akizungumza na vijana wa Hamasa wa Kata ya Maendeleo alipofika kuzindua mradi wa kujiwezesha kiuchumi wa kufyatua tofali.





Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson akishiriki kufyatua tofali katika mradi wa Vijana wa Kata ya Maendeleo

Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt Tulia Ackson amewataka Madiwani wa kata 36 za Jiji la Mbeya kubuni miradi endelevu itakayoweza kuyasaidia kiuchumi makundi ya vijana katika kata zao.

Dkt Tulia ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ameyasema hayo wakati akizindua mradi wa kufyatua tofali katika kata ya Maendeleo uliolenga kuwanufaisha Vijana wa Hamasa wa Chama Cha Mapinduzi CCM wa kata hiyo.

‘’Miradi namna hii itawawezesha vijana ambao wamechangia ushindi wa chama chetu kwenye uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba…tuige mfano wa Kata ya Maendeleo kuwasaidia vijana wajiwezeshe kiuchumi’’amesema Dkt Tulia.

Dkt Tulia ameahidi kumuunga mkono Diwani wa Kata hiyo Issa Salmin kwa kuwasaidia  Vijana hao Saruji mifuko  30 na lori tano za mchanga.