HAKIMU ATIWA MBARONI ANASWA NA TAKUKURU MBEYA

Na Ripota wa Mbeya Yetu

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imemnasa na kumburuza Mahakamani Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Igurusi Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya Harrison Makinda na kushtakiwa kwa makosa ya Udanganyifu na uvunjifu wa uaminifu kwa Mtumishi wa Umma.

Mashtaka hayo yanayounganishwa kwa pamoja kwa shauri la jinai nambari 272/2020 ambalo kosa la kinyume cha kifungu cha 120,kutoa taarifa za uongo kwa Mtumishi wa umma kinyuma cha kifungu 122 na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kinyume na vifungu vya 302 na 302 kanuni ya adhabu sura ya 16 ya mwaka 2002.

Akitoa taarifa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya Julieth Matech amesema Mshitakiwa Makinda mnamo Mei,16 2019 aliwasilisha nyaraka yenye maelezo ya Uongo kwa Afisa wa Gereza la Rujewa wilayani Mbarali akimtaarifu kwamba  mshitakiwa aliyetiwa hatiani na kutumikia kifungo cha miaka mitano jela anatakiwa kutolewa  gerezani.

Matech amefafanua kuwa Hakimu huyo alidai kuwa Mshitakiwa huyo aliyetakiwa kulipa faini ya LAKI MOJA na fidia ya Shilingi Laki 6 tayari imeshalipwa ilhali akijua wazi kuwa si kweli na kuwa hukumu aliyoiandika Hakimu huyo kwenye shauri nambari 99/2019 kwa mshitakiwa haikuwa na adhabu ya faini hiyo.

Aidha Matech amesema kuwa Hakimu huyo alifanya udanganyifu kwa kumlipisha ndugu wa mshitakiwa kiasi cha Shilingi LAKI 6 bila kumpatia stakabadhi yoyote ya malipo.

Mshitakiwa amekana Mashtaka hayo na Mahakama imemwachia kwa dhamana ambapo shauri hilo limepangwa kusikilizwa upande wa Jamhuri Januari 20 ,2021.

TAMATI.