KAMPUNI YA MAJINJAH YAANZISHA KIWANDA CHA KAHAWA ''MAJINJAH COFEE CURRING''

Na Ripota wa Mbeya Yetu,Mbozi.

Katika kuunga mkono Serikali ya awamu ya Tano kuelekea Nchi ya Viwanda Kampuni ya Majinjah Logistics Limited inayojishughulisha zaidi na Usafirishaji wa Mabasi ya Abiria na Mizigo imeamua kuelekeza nguvu zake katika uwekezaji wa Viwanda na Kilimo.

Majinjah Logistics Company Limited ni kampuni  yenye makampuni mengi baadhi yake yakiwemo  kampuni ya  usindikaji wa Maji safi ya Kunywa ya Tukuyu Springs Water iliyopo Kibisi Wilayani Rungwe,Kiwanda cha Usindikaji wa Sembe cha Majinjah Mill kilichopo Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani na Mabasi ya Usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia Majinjah Special mikoa mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Majinjah Logistics Limited Alinanuswe Ahobhokile Kabungo ‘’Mzee Majinjah’’ anaeleza Majinjah Logistics imeanza kujikita kwenye shughuli za Kilimo na uwekezaji wa Viwanda, kwa sasa imeanza katika uwekezaji kwenye uanzishwaji wa kiwanda cha Kusindika Kahawa katika Kijiji cha Igamba wilayani Mbozi Mkoani Songwe.

Mzee Majinjah anasema sera ya Uwekezaji ambayo ni maoni ya Rais Dkt John Magufuli imehamasisha wawekezaji kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya uwekezaji wa Viwanda na kuwa Majinjah imeamua kujenga kiwanda cha Kahawa karibu kabisa na wakulima maeneo ya vijijini.

Anafafanua kuwa uwekezaji katika mkoa mpya wa Songwe utazidi kuufanya mkoa huo kushindana na hata kuipiku mikoa ya zamani kutokana na mkoa huo kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara.

Anasema Wakulima wa Zao la Kahawa Wilayani Mbozi wataanza kunufaika kwa uwepo wa kiwanda hicho karibu na maeneo yao na kuwa awali kahawa ilikuwa ikisafirishwa kwa ajili ya ukoboaji Jijini Mbeya.

Kuhusu kuwasaidia wakulima wazalishe Kahawa bora          Mzee Majinjah amesema watashirikiana na wakulima katika kutoa elimu ya Kilimo bora na kwa kupitia kikundi cha Wakulima wa Kahawa Mawanga AMCOS wataketi na kuhamasishana kilimo bora chenye tija.

Katika kuhakikisha wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbozi wanaepuka kupunjwa kwa kuuza mazao yao yakiwa shambani KATA KICHWA wanachama wa MAWANGA  AMCOS wamehamasishwa kutouza kahawa yao mapema kuepuka kudhulumiwa wakati wa mavuno.