Shirika la Umeme TANESCO Mkoani Songwe limetekeleza agizo la Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo kwa kufunga Transfoma kwenye Kiwanda kipya cha Kukoboa Kahawa cha Majinjah Coffee Curing Limited kilichopo Igamba Wilayani Mbozi Mkoani Songwe.


Agizo hilo limetekelezwa ikiwa imepita wiki moja tu baada Katibu Mkuu Chongolo kuipa siku 21 TANESCO kuhakikisha Transfoma hiyo inafungwa kiwandani hapo ili kusaidia mwekezaji kuanza uzalishaji ambao utachangia ajira kwa wananchi na kuongeza uchumi wa Taifa.

Awali Msimamizi wa miradi wa Kampuni ya Majinjah Logistics Mhandisi James Mgeni alitoa maelezo mbele ya Katibu Mkuu juu ya changamoto za kiutendaji zinazosababisha kiwanda kuchelewa kuanza usalishaji kwa  kukosa Transfoma.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo katika hitimisho la ziara yake Mkoani Songwe alitoa maagizo na kusisitiza Shirika la Umeme TANESCO kupeleka Transfoma kiwandani hapo ndani ya siku 21 ili mwekezaji Majinjah Coffee Curing aanze uzalishaji.

Kwa upande wake Mwekezaji Alinanuswe Kabungo (Mzee Majinjah) ameshukuru jitihada za kiutekelezaji zinazosimamiwa na CCM na kuhamasisha utendaji uliotukuka uliofanywa na Shirika la Umeme TANESCO Mkoani Songwe.

Mzee Majinjah amemshukuru kipekee Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwa kuona umuhimu wa uwekezaji ambao unasaidia kuliletea tija Taifa kiuchumi sanjari na kuongeza ajira kwa wananchi.

Kiwanda hicho kipya cha Majinjah Coffee Curing kipo katika kijiji cha Mawanga Kata ya Igamba wilayani Mbozi Mkoani Songwe kina Uwezo wa kukoboa tani 72 kwa siku na teknolojia ya kisasa itakayomrahisishia mkulima kukobolewa kahawa yake kuweka madaraja na kufanya usindikaji.