Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewatoa hofu wakazi wa Gezaulole mkoani Morogoro juu ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo hasa baada ya Wizara kuanza kutoa fedha za utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji katika eneo hilo.

 

Mahundi amesema kero ya maji itakwisha baada ya kukamilika kwa mradi wa maji utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 14. Mradi huo unatekelezwa kufuatia mradi wa awali uliotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 400 kupata changamoto ya chanzo chake cha maji kutokuwa na maji ya kutosha.

 

Ametoa wito wa kutunza vyanzo za maji akiwataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kikiwemo kilimo ambacho husababisha ukame na uharibifu wa mazingira.

 


Kwa upande wake Meneja RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi John Kisengi amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji licha ya juhudi zinazofanywa za kuchimba visima.

 


Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amesema zaidi ya miaka mitano kero ya maji haijatatuliwa ilhali akimpongeza kwa kwa kuwa Naibu Waziri wa kwanza kutembelea eneo hilo.

 

Aidha ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa maji ili kulinda vyanzo vya maji kutokana na wakulima na wafugaji kuvamia vyanzo hivyo.