MAJALIWA APIGA STOP WAANDISHI,WALINZI BINAFSI KATIKA OFISI ZA UMMA.

  

Na Mwandishi Wetu Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Mawaziri na Manaibu Waziri waepuke kuwa na matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa  chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali.

 

“Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao. Zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo.”


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa Oktoba 29,2021  alipokuwa akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper jijini Dodoma. Mafunzo ambayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

 

Kadhalika amewaagiza Mawaziri na Naibu Waziri wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukomesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora.


“Ninapenda kuwakumbusha kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote.”

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.