Tanzania ni mwanachama wa Bonde la Mto Nile. Nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Bonde la Mto Nile ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Misri, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Uganda pamoja na nchi ya Eriteria ambayo ina hadhi ya uangalizi (observer).

 

Katika kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ya Bonde la Mto Nile, Baraza la Mawaziri wa Bonde hilo hufanya mikutano kila mwaka. Kufuatia ratiba hiyo, Mkutano wa 29 wa Baraza la Mawaziri wa Maji kutoka nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile umefanyika leo tarehe 26 Novemba, 2021 jijini Juba Sudan Ya Kusini ambapo Mhe. Maryprisca Winfried Mahundi Naibu Waziri wa Maji ameiwakilisha Tanzania kwenye Mkutano huo kwa niaba ya Mhe. Jumaa Hamidu Aweso Waziri wa Maji.

 

Mkutano huo ni kiungo muhimu katika kuendeleza ushirikiano wa Bonde la Mto Nile pamoja na Tanzania kuendelea kusimamia maslahi ya Taifa letu ya matumizi ya maji ya Ziwa Victoria. Vile vile, Tanzania imetumia  fursa ya Mkutano huu wa leo  kuendelea kuzishawishi nchi za Burundi na Sudan ya Kusini kuridhia Mkataba wa kuanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Nile (Cooperative Framework Agreement) ambao utakuwa muhimili katika kuendesha shughuli za Bonde la Mto Nile.

 

Katika Mkutano huo Waheshimiwa Mawaziri wa maji kutoka nchi za Bonde la Mto Nile wamejadili na taarifa ya utendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Mto Nile, imepitisha mpango kazi na Bajeti ya Bonde la Mto Nile kwa mwaka 2021/2022. Vile vile kwa Pamoja Baraza la Mawaziri wa Bonde la Mto Nile wamekubaliana kuwa Mkutano wa wakuu wa nchi za Bonde la Mto Nile (Nile Head of State Summit) kufanyika Sudani Kusini. Tanzania pia imekuibali kuwa mwenyeji wa sherehe za kuadhimisha siku ya Nile zinazofanyika kila mwaka tarehe 20 mwenzi Februari.

 

Kupitia ushirikiano katika usimamizi na uendelezaji wa Bonde la Mto Nile, Tanzania inaendelea kupata faida mbalimbali ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rusumo ambapo Tanzania itapata megawati 27 kati ya 80 zitakazozalishwa. Vile vile Tanzania inafaidika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa kutathmini uhusiano wa maji juu na chini ya ardhi katika eneo la Bonde dogo la Mto Kagera, ujenzi wa vituo vya kupima wingi na ubora wa maji na miradi mingine mingi.

 

Mkutano wa 29 wa Baraza la Mawaziri wa Maji kutoka nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile Umemalizika kwa mafanikio makubwa ikiwepo Misri kukubali kurudi na kuendelea kushirikiana na nchi nyingine za Bonde la Mto Nile baada ya miaka kadhaa ya kujitoa kwa sababu ya kutokukubaliana kwenye kipengele cha 14 cha Mkataba wa kuanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Nile (Cooperative Framework Agreement).