WATOTO 23 WAFANYIWA UPASUAJI MKUBWA WA MOYO KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU YA MOYO INAYOFANYIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)


Jumla ya watoto 23 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo (Congenital Heart Disease) wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Upasuaji huo wa moyo unafanywa na  Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na  wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saud Arabia.

Matibabu yanayotolewa katika kambi hii ni kuziba matundu ndani ya moyo,  kuzibua njia za mishipa ya damu ya moyo iliyobana, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo iliyokaa vibaya na kuzifanyia marekebisho Valvu za moyo kwa kuzikarabati au kubadilisha kabisa na kuweka za chuma. Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri.

Hii ni mara ya pili kwa wataalamu hawa kuja katika Taasisi yetu kwa ajili ya kufanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto. Mara ya mwisho walikuja mwaka 2019 kabla ya janga la ugonjwa wa UVIKO – 19 lililozuia ujio wao kwa mwaka 2020. Wataalamu hawa wamepongeza jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu katika kipindi cha miaka miwili ambacho hawakupata nafasi ya kuja nchini.Pia wamewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kuongeza ujuzi wa kufanya upasuaji wa moyo.

Kambi hii ya siku 10 ambayo inaenda sambamba na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wataalamu wetu wa kitanzania na wageni ilianza  tarehe 11/12/2021 na itamalizika tarehe 20/12/2021.


 Imetolewa na:        

 Anna Nkinda

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

14/12/2021