MWEF KUJENGA HOSTEL WATOTO WA KIKE MBARALI,DIWANI AKABIDHI GARI NA PIKIPIKI.

Taasisi ya Maryprisca Woman Empowerment Foundation inatarajia kujenga Hostel kwa ajili ya watoto wa kike kata ya Mawindi wilayani Mbarali mkoani Mbeya ili kuchangia ufaulu na changamoto za masomo wanazokumbana nazo watoto wa kike wilayani humo.

Hayo yamejiri Disemba 17,2021 wakati wa makabidhiano ya gari aina ya Noah na  Pikipiki  nne zilizotolewa na Diwani wa kata ya Mawindi Sadiki Kimelenyi zenye thamani ya jumla ya Sh Milioni 26.5 kwa ajili ya kusaidia huduma za Afya mbele ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Mhandisi Maryprisca Mahundi.

Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa anayewakilisha wanawake mkoa wa Mbeya amesema kuwa ameguswa na hamasa ya kuchangia maendeleo ya jamii zilizofanywa na Diwani wa kata hiyo Kimelenyi.

‘’Nampongeza sana Mheshimiwa Diwani, amefanya jambo la kuigwa kwa kuokoa uhai wa wananchi wa kata yake,nitazifikisha taarifa hizi kwa Waziri wa Afya’’ amesema Mhandisi Maryprisca.

Mhandisi Maryprisca amesema kuwa kwa upande wake ataunga mkono jitihada hizi za kusaidia maendeleo ya kata hiyo kwa kujenga Hosteli kwa ajili ya Watoto wa kike katika mwaka ujao wa fedha ili kuongeza ufaulu.

‘’Kupitia taasisi ya Maryprsisca Woman Empowerment Foundation, tutajenga Hosteli moja kwa ajili ya watoto wa kike na Mwenyezi Mungu atakapotujaalia kwa kushirikiana na Diwani tutaangalia namna kupata Hosteli kwa ajili ya watoto wa kiume’’amesema.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mawindi Sadiki Kimelenyi amesema ametoa vyombo hivyo vya usafiri kusaidia huduma kwa wakazi wa sehemu mbalimbali kutoka ndani na nje ya kata ya Mawindi na wilaya ya Mbarali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Missana Kwangura amempongeza Diwani wa kata hiyo na kusema kuwa msaada huo utarahisisha huduma katika kituo cha Afya kata ya Mawindi na Zahanati nne zilizopo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali Hashimu Mwalyambi  na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamemshukuru Diwani kwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020.