Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi(Mb)ameshuhudia utiwaji saini wa Mktataba wa kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji mto Kiwira wenye thamani ya shilingi bilioni 2.216 baina ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mbeya na Kampuni ya Lahmeyer Consulting Engineers(T)Ltd ya Dar Es Salaam.


Hafla hiyo imefanyika ukumbi wa Mamlaka hiyo ikihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera,Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Dkt Anjelina Lutambi,Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt Rashid Chuwachuwa,Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt Vicent Anney,Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune,Mwenyekiti wa Bodi Edina Mwaigomole,Mwenyekiti wa CCM Mbeya Vijini Akimu Mwalupindi,Mwenyekiti CCM Jiji Afrey Nsomba na Menejimenti ya Mamlaka ya Maji.


Mhandisi Mahundi amesema hana shaka na mhandisi mshauri kwani amesimamia miradi mingi nchini kwa ufanisi mkubwa hivyo ni matumaini yake hata mradi huu atausimamia vizuri kuhakikisha mkandarasi anatekeleza kama ilivyokusudiwa ili kutomwangusha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa fedha nyingi kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani.


Aidha amempongeza Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya ambaye amekuwa akiusemea mradi mara kwa mara na sasa umefikia hatua ya kutekeleza.


"Katika uongozi wa Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso tulikuta miradi kichefuchefu 120 ya maji lakini mpaka sasa miradi 80 imekwelisha na inatoa maji na hiyo iliyosalia nayo pia itakwisha",alisema Mahundi.


Amesema mradi ukikamilika utatoa maji zaidi ya asilimia mia moja na ziada itasambazwa katika Wilaya zote na Mkoa jirani wa Songwe.


"Hivi karibuni serikali imeingia mikataba na wazabuni mbalimbali ukiwemo awamu ya pili mradi wa Matwiga ambao utapunguza kero ya maji Wilaya ya Chunya",alisema Mahundi.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera mbali ya kushukuru serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mradi huo amesema ofisi yake itahakikisha inatoa ushirikiano ili mradi huo usiwe na kikwazo.


Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira CPA Gilbert Kayange amesema mbali ya kuanza mradi huo pia Mamlaka inatekeleza miradi saba Jijini Mbeya kati yake minne imekamilika na ikikamilika mbali ya kupunguza changamoto ya maji pia itasaidi kuongeza  mapato.


Mwenyekiti wa Bodi Edina Mwaigomole ameishukuru serikali na Mawaziri kwa namna wanavyofuatilia utekelezaji wa miradi sambamba na kuomba mhandisi mshauri kumpata mkandarasi mapema ili mradi ukamilike kwa wakati.


Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt Rashid Chuachua na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe wamesema wananchi wanaopitiwa na mradi huo wawe wanufaika wakubwa wa maji na kazi zitakazotolewa na mkandarasi.


Mwenyekiti wa CCM Mbeya Jiji Afrey Nsomba amempongeza Spika wa Mbunge wa Mbeya Dkt Tulia Ackson kwa ufuatiliaji na pia Naibu Waziri wa Maji kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi.


Mradi wa maji Kiwira unatarajiwa kukamilika mwaka 2024 hivyo kilio cha maji jijini Mbeya kitakuwa historia.