*WATUMISHI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAHIMIZWA KUUTANGAZA UTALII WA NDANI NA NJE NCHI.* 


DODOMA.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja amewataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wawe mstari wa mbele katika kuhamasisha na kutangaza utalii ili kuvutia watalii wengi zaidi kwenda kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini.


Mhe. Mary ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo na Taasisi zake ambapo amesema  kuwa iwapo kila mtumishi ataamua kutumia nafasi yake kutangaza utalii mwamko wa Watanzania kutembelea vivutio vilivyopo utaongezeka.


‘’Tunatakiwa sisi wenyewe tuoneshe mfano kwa kutafuta masoko na kuhamasisha Utalii, kutafuta mikutano mbalimbali inayo fanyika maeneo ije kufanyika Tanzania tuuze huduma za kumbi zetu za Kimataifa, bidhaa na bidhaa zetu kupitia hiyo mikutano” Amesema Mhe. Mary Masanja.


Amesema kuwa kupitia kuuza fursa hizo na mazao mbalimbali ya Utalii yaliyopo hapa nchini hususani mikutano ya Kimataifa itakuwa kichocheo kwa watalii wengi kuhamasika kufika kwenye vivutio vilivyopo.


Mhe. Mary Masanja amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila wizara na taasisi kutangaza utalii hatua itakayosaidia kuongeza Pato la Taifa kupitia watalii wanaokuja kutembelea vivutio hivyo hapa nchini.


Aidha, katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja ametoa wito kwa Wanawake wote wa Wizara hiyo kuyatumia Maadhimisho yajayo ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayoadhimishwa  Machi 8 mwaka huu kupaza Sauti zao kwa kuhamasishana kutangaza Utalii wa ndani na kutembelea vivutio vilivyopo.


‘’Sasa hivi tumekuwa na matukio ya watu kujiua, tunataka tupunguze tatizo hili kwa kufurahi kukutana pamoja ,kubadilisha mawazo . Tunataka kuanzia tarehe 1 mpaka 8 mwezi Machi mwaka huu sisi wenyewe tuutangaze utalii wetu’’ Amesisitiza 


Katika hatua nyingine, Mary amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa uadilifu na upendo na kuepuka mambo yayonarudisha nyuma utendaji wao mahali pa kazi huku akiwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa ushirkiano  ili Sekta ya Utalii izidi kusonga mbele.