UTPC YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI MBEYA JUU YA ULINZI NA USALAMA WA VIFAA VYA KAZI



Baadhi ya Waandishi wa Habari Mkoani Mbeya wamepatiwa mafunzo ya usalama wa vifaa vya kazi sambamba na matumizi ya mitandao ya kijamii.


Mafunzo hayo yamefanyika ofisi za klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya(MBPC) mafunzo yaliyoratibiwa na Muungano wa klabu za Waandishi wa Habari nchini(UTPC).


Mkufunzi wa mafunzo hayo Joseph Mwaisango amewataka waandishi kuvitumia vyombo vya kazi kwa umakini kama camera,laptop,recorder na email kwa umakini ili taarifa zao zisidukuliwe.


Amesema waandishi waache tabia za kuazimana vitendea kazi kwani baadhi wanaweza kuzidukua taarifa na kuzisambaza bila kujua endapo utaamwachia nyuwila ya email yako.


Aidha kutokana na umuhimu wa masomo hayo Mwaisango amewataka waandishi kujifunza kila siku ili wafanye kazi kwa uweledi na usalama kwani habari zozote zinazotoka zipo zinazowafurahisha watu nyingine zinawaumiza watu hivyo waandishi wajali usalama wao.


Waandishi walionufaika na mafunzo hayo ni pamoja Grace Mwakalinga,Elizabeth Nyivambe,Nebart Msokwa,Keneth Mwakandyali na Ezekiel Kamanga.


Grace Mwakalinga mbali ya kushukuru kupatiwa mafunzo ameiomba UTPC kutoa mafunzo kwa waandishi mara kwa mara.


Naye Nebart Msokwa amesema mafunzo kama hayo yatolewe ana kwa ana badala ya mafunzo kutolewa kwa njia ya mtandao.


Msokwa amesema hata vifaa endapo vinapelekwa kwa mafundi ni vema nyaraka zikahifadhiwa ili kuepusha fundi kuzidukua na kuzisambaza.


Aidha mafunzo ya ana kwa ana yatawapa uwanda mpana wa kuuliza maswali na kujibiwa sambamba na mazoezi ya vitendo yatakayowapa waandishi uelewa mkubwa.


Waandishi waliopatiwa mafunzo nao watawafundisha waandishi wengine ili kupanua wigo wa waandishi Mkoani Mbeya ambapo Mkoa wa Mbeya una zaidi ya Waandishi mia moja wakiwemo wa Magazeti,Radio,Runinga na Mitandao ya kijamii.


Waandishi wengi wamekuwa na changamoto ya vitendea kazi hivyo kuwalazimu kushirikiana vifaa suala ambalo ni hatari pindi inapotokea mmoja kufanya uhalifu kupitia kifaa cha mwenzake bila yeye kujua.