Mwakilishi wa Chama cha Watoa Huduma za Utalii (TLTO) Sam Dia akifuatilia uzinduzi wa Maandalizi ya Onesho la Swahili International Tourism Expro 2023 uliofanyika tarehe 25 Aprili, 2023 Serena Hotel jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Damasi Mfugale (mwenyewe shati la bluu Bahari) katika picha ya Pamoja na wadau wa utalii kwenye uzinduzi wa Maandalizi ya Onesho la Swahili International Tourism Expro 2023 uliofanyika tarehe 25 Aprili, 2023 Serena Hotel jijini Dar es Salaam.
Baadhii ya Wajumbe wa Menejimenti ya Bodi ya Utalii Tanzania na Wadau wa Utalii wakati wa hafla ya Uzinduzi wa onesho la S!TE uliofanyika katika Hoteli ya Serena.
Na Mwandishi wetu, DSM
Bodi ya Utalii Tanzania inatarajia kufanya onesho la Saba la Swahili International Tourism Expro – S!TE ikiwa ni mikakati ya kutangaza utalii na kuwasaidia wafanyabiashara wa utalii wadogo na wa kati kuweza kupenya katika masoko ya kimataifa kwa gharama nafuu.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Damas Mfugale ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya onesho la S!TE 2023 na kusema kuwa Onesho hilo litafanyika kuanzia tarehe 06 hadi 08 Oktoba katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Amesema kauli mbiu ya onesho itakuwa ni “Kukuza Utalii Jumuishi na Endelevu” na litahusisha utangazaji wa bidhaa mbalimbali za utalii, jukwaa la uwekezaji, semina kuhusu masuala ya utalii na masoko na mikutano ya wafanyabiashara ya utalii.
“Msimu huu tunatarajia kuleta waoneshaji 200 na wanunuzi wa kimataifa takribani 150 kutoka masoko ya ndani ya utalii ya msingi na yale yanayochipukia hususani ya kimataifa” amesema Bw. Mfugale
Ameongeza kuwa onesho hilo litasaidia kuwa chachu ya kuongeza watalii kwa kuwashirikisha Watanzania wenyewe kutangaza fursa za utalii na uwekezaji kwa kuwakutanisha na wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa za utalii (Buyers) kutoka mataifa mbalimbali.
“Maonesho haya yana miaka 7 toka yameanzishwa mwaka 2014 na yamekuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni kuongezeka kwa idadi ya waoneshaji na wanunuzi wa kimataifa, kutoka waoneshaji 40 hadi 170 na wanunuzi wa kimataifa kutoka 24 hadi 333 kufikia mwaka 2022” amesema Mfugale
Ametoa rai kwa wadau wa utalii waliopo ndani na nje ya nchi hususani Mawakala wa biashara za utalii, watoa huduma za malazi, mawakala wa safari na waongoza watalii kuchangamkia fursa za kiuchumi na za kijamii zitakazojitokeza kupitia onesho hilo.
Bw. Mfugale amesema kuwa kutakuwa na punguzo la 10% kwa wadau watakaojisajili mapema ndani ya siku 14 tangu kuzinduliwa kupitia tovuti ya site.tanzaniatourism.go.tz ili kutoa fursa ya wadau kujisajili mapema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki CRDB, Abdulmajid Nsekela amepongeza Bodi ya Utalii kwa kuwa na maono ya kuanzisha onesho hilo kwa kuwa litawapa nafasi ya kutangaza maeneo ya kuwekeza katika sekta ya utalii.
Amesema kuwa onesho hilo ni muendelezo Royal Tour ambayo imefanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu na pia itoa fursa kwa benki ya CRDB kutoa huduma mbalimbali za kifedha kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa za kitalii.
“Unapokuwa unatangaza huduma kidigitali hata anayeihitaji ataipata kidigitali kwa sababu hiyo benki ya CRDB kazi yetu ni kuweka mifumo ya kiulipaji vizuri ili mtu aweze kulipa moja kwa moja kutoka sehemu alipo ili CRDB ipate fedha yake na Serikali ipate kodi” amesema Nsekela.
Naye Meneja wa Mauzo wa Serena Hotel, David Semu amesema kuwa wao kama wadau wa utalii wanatarajia kupata fursa ya kuonana na Makampuni na Mawakala wa Utalii kutoka sehemu mbalimbali za duniani ambayo itasaidia kukuza utalii.
Bw. Semu amesema kuwa kwa muda ambao wageni watakaokuwepo watapata fusra ya kujiongezea kipato katika huduma za malazi, chakula na usafiri kwa sababu maonesho hayo yanawagusa hata wananchi wa kawaida.
0 Comments
Post a Comment