BILIONI 16 KUNUFAISHA VIJIJI VISIVYOKUWA NA MAJI SONGWE


Na Ripota wa Mbeya Yetu, Songwe

SONGWE: Katika kuongeza asilimiaya upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 73 hadi asilimia 100, Mkoa wa Songwe umepata jumla ya Shilingi Bilioni16.4 ikiwa ni fedha za utekelezaji wa mradi wa maji Vijijini za mpango maalumu wa Lipa kwa Matokeo PfoR utekelezaji unaotarajia kuanza hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brige. Gen Nicodemus Mwangela amesema miradi ya Maji inapojengwa na kukamilika inaongeza asilimia ya upatikanaji wa Maji kwa Wananchi Vijijini.

‘’Nitoe Wito kwa Jamii kutunza vyanzo vya Maji na kuilinda Miradi ili Wananchi wapate Maji kwa muda mrefu,’’amesema Mwangela.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini RUWASA Mkoa wa Songwe Mha ndisi Charles Pambe, amesema kitendo cha Utekelezaji wa miradi ya Maji kupitia Force Account kumesaidia kuwajengea uwezo Wataalamu kutekeleza miradi kwa asilimia 100.

Mhandisi Pambe amebainisha kuwa RUWASA imejipanga kutekeleza miradi hiyo ndani ya miaka mitatu ili vijiji vyote visivyokuwa na maji katika mkoa wa Songwe vianze kutoa maji.

Pambe amefafanua kuwa  Mkoa wa Songwe ulipata kiasi cha Tsh Bilioni 5.6 za PfoR kama mbegu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi lakini kutokana na  mkoa kufanya vizuri kwenye utekelezaji zimeweza kuzalisha mara 3yake jumla ya Tsh Bilioni 16.4.