NAIBU WAZIRI WA MAJI ‘’AMUONYA’’ WAKALA WA RUWASA NYUMBANI KWA
JPM
Na Ripota wa Mbeya Yetu, Chato
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa onyo kwa Meneja wa Wakala wa MajiSafi
na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Chato Mhandisi Andrew Kilembe kwa
kushindwa kutatua kwa wakati kero ya ubovu wa mita za maji zilizowekwa katika
mradi wa maji wa Imalabupina Inchwankima na kusababisha wananchi wa eneo hilo
kukosa maji kwa siku kadhaa.
Ametoa onyo hilo baada ya kupokea malalamiko toka kwa wananchi
wakati akikagua mradi huo unahohudumia wakazi wa vijiji hivyo.
Amesema wananchi wanakosa huduma ya maji kwa sababu ya viongozi
kufanya kazi kwa mazoea na kushindwa kutatua kero zinazojitokeza kwa wakati.
“Natoa onyo na naomba fuatilieni hilo tatizo linalosababisha
wananchi wasipate maji kwa wakati maeneo mengine yanatoa maji, na hakikisheni
hizo mita zinazosumbua zinabadilishwa haraka ili kuondoa kero hiyo na wananchi
hawa wapate maji”, amesema Mhandisi Mahundi na kusisitiza kero zote ikiwemo
matatizo ya umeme yasisubiri viongozi.Hata hivyo pamoja na kumuonya Meneja huyo, amempongeza kwa hatua
yake ya kuamua kutumia shilingi milioni 311 kukarabati miundombinu ya mradi wa
maji Kasenga ambao ulichakaa na kuacha kutoa maji kwa muda mrefu.Katika ziara yake ya kukagua miradi ya maji mkoani Geita Naibu
Waziri alikagua pia mradi wa maji wa Katoro Buseresere ambao utekelezaji wake
unaendele vizuri na mradi huo ukikamilika utahudumia wananchi 20,000 wa kata ya
Buseresere, Katoro, Ludete na Nyamigota.
0 Comments
Post a Comment