DANGOTE YAKANUSHA TAARIFA YA AJIRA ILIYOSAMBAA MITANDAONI

Na Mwandishi Wetu

Uongozi wa Kampuni, Kiwanda cha Saruji Dangote mkoani Mtwara Dangote Cement Factory kimekanusha taarifa iliyosambazwa mitadaoni kwamba kampuni hiyo imetoa wito kwa nafasi mbalimbali za ajira ilizotangaza hivi karibuni.

Mara baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo Mbeya Yetu Online Tv iliwasiliana na Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Dangote Rachel Singo ambaye alisema kuwa taarifa hizo si za kweli bali ni za kughushi zilizolenga kuwatapeli Watanzania.

Amefafanua kuwa mara baada ya kusambaa taarifa hizo kwa njia ya mitandao Kampuni hiyo ikasambaza taarifa hiyo kwa kuweka muhuri wa moto uliosomeka FAKE NEWS na kusambaza kwa njia hiyo hiyo ya mitandao ili kuwafikia wananchi.

Taarifa hiyo ya wito wa usaili iliyochapishwa na kusambazwa mitandaoni iliwataka waliochaguliwa kuwepo kwenye awamu ya kwanza ya usaili kufika ukumbi wa Royal Village Hotel Jijini Dodoma na Ukumbi wa Pentekostal Ligula mkoani Mtwara.

Aidha taarifa hiyo iliwataka waliochaguliwa kwa Dodoma na Mtwara kuwasili  tarehe 4 Novemba 2021 saa 12 jioni ambapo mwisho wa kuwasili ulianishwa katika taarifa hiyo kuwa ni Saa 2 usiku ya tarehe hiyo hiyo.