Naibu Waziri wa Maji
Mhandisi Maryprisca Mahundi ameanza ziara ya siku mbili katika Wilaya ya
Malinyi Mkoa wa Morogoro yenye lengo la kukagua miradi ya maji sambamba na
kuwatambulisha Wakandasi watano waliochaguliwa kutekeleza miradi ya maji katika
Wilayani humo.
Miradi hiyo mitano ni
Misegese, Itete Njiwa, Igawa, Ngoheranga na Uchimbaji wa visima virefu 14
ambapo utekelezaji huo utagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 2.8. Katika miradi
hiyo mitano, mradi wa maji Ngoheranga unatekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 kiasi
cha Shilingi Milioni 641.
Mahundi amesema katika
mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya shilingi bilioni tatu zitatumika kwa ajili ya
miradi mbalimbali katika Wilaya ya Malinyi.
Ushirikiano baina yake
na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na watumishi wa Wizara ya maji utaifanya
Serikali kufikia malengo yake kwa nia ya kuwaondolea kadhia ya upatikanaji wa
majisafi na salama.
Aidha amemshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa
kuelekeza fedha nyingi katika miradi ya maji ilu kuhakikisha wananchi wa
Tanzania wanapata majisafi, salama na ya uhakika hii ni katika kutimiza ile
azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Mbunge
wa Jimbo la Malinyi Mheshimiwa Antipas Mgungusi mbali ya kumshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Wizara ya
Maji kwa ujumla amewatoa hofu wananchi kwa namna walivyokumbukwa katika miradi
mbalimbali ya maji hivyo wananchi kuendelea kuiamini Serikali.
Mhe. Mgungusi amewapongeza Mawaziri na watumishi wote wa Wizara kwa namna wanavyochukua hatua
za kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maji nchini.
0 Comments
Post a Comment