Umuhimu wa Kusajili Tovuti au Wavuti Yako na Kikao cha DOT TZ
Na Mwandishi wetu
Ni
muhimu kusajili tovuti yako kwa kutumia kikoa cha dot tz (.tz) katika matumizi
ya intaneti ili kutoa utambulisho wa kitaifa, na kukuza uchumi wa Taifa.
Kikoa cha dot tz (.tz) ni
nini? ni rasilimali ya nchi (Tanzania) kwa ajili ya mawasiliano kwenye mtandao
wa intaneti kupitia tovuti au barua pepe. Kila nchi imepewa utambulisho pekee
mtandaoni.
Pamoja
na jitihada ambazo zinafanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na hapo awali
tzNIC bado kampuni nyingi na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa na
kufanya kazi Tanzania ni watumiaji wa vikoa vingine kama .com na .org.
Meneja Usimamizi wa Rasilimali za Mawasiliano na Teknolojia
wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mwesigwa Felician akizungumzia
umuhimu wa biashara na taasisi za serikali kusajili tovuti na utambulishi wa
barua pepe zao kwa kikoa cha dot tz anasema kusajili tovuti au barua pepe kwa kutumia
kikoa cha Tanzania kuna faida mbalimbali ikiwemo kupunguza gharama za mawasiliano,
kuongeza wigo wa ulinzi wa taarifa na kukuza uchumi wa nchi kutokana na fedha
zinazotumika kusajili vikoa hivyo kubaki nchini.
“Kwa
wenzetu wanaotumia mtandao tunashauri wasajili majina yao kama vile tovuti na
barua pepe kwa kikoa cha dot tz, kwa sababu vikoa vingine kama vile dot com
haviwezi kuwa na msaada kwa Tanzania kwani fedha zinazotumika kusajili vikoa
hivyo hupelekwa kwenye mataifa hayo ila ukijisajili kwa kikoa cha dot tz fedha zinabaki
hapa nchini, usalama wa taarifa zako au taasisi yako unakuwa wa uhakika, na
taarifa zako zinapatikana popote duniani, zaidi ya hayo jambo hili ni takwa la
kisheria.” Alibainisha Mwesigwa.
Kielelezo cha vikoa kwa nchi mbalimbali duniani; Tanzania
ikionekana kwenye duara, ambapo utambulisho
wa nchi ni kikoa cha .tz. Picha: Mtandao
Kila
anwani ya mtandao, inacho kikoa kinachoishia, kinachojulikana pia kama kikoa
cha ngazi ya juu cha nchi (country code top-level domain ccTLD). Vikoa vya viwango vya juu vya msimbo wa nchi
(ccTLDs) hutumika kuonyesha uhusiano wa tovuti na nchi au eneo mahususi (yaani
.uk kwa Uingereza au .eu kwa Umoja wa Ulaya) na kwa hivyo hujulikana kama msimbo
wa ki-nchi.
Mbali
na kuwezesha fedha kubaki nchini suala ambalo linayo manufaa kwenye uchumi, Felician
alisisitiza kuwa kikoa cha dot tz kinakupa utambulisho wa kitanzania katika
Mtandao wa Intaneti; kinawezesha biashara yako kupatikana sehemu yoyote duniani
kupitia mtandao wa Intaneti; aidha, matumizi ya kikoa cha .tz yanachangia
kupunguza gharama za Mawasiliano kupitia Mtandao wa Intaneti.
“Kwa
kweli faida za matumizi ya kikoa cha dot tz ni nyingi; mbali na hayo
niliyoyaeleza hapo awali mengine ni pamoja na kikoa hiki kinatoa ushindani sawa
wa kibiashara mtandaoni; kutoa au kuwezesha kipaumbele cha upatikanaji wa
biashara zilizopo Tanzania mtandaoni hapa namaanisha yale mapendekezo biashara
au huduma kieneo, mara nyingi mtandao utakuelekeza kwenye tovuti za nyumbani
kwanza kabla hujafika huko kwingine, hii inakuwezesha kuwafikia wadau wako wa
ndani ya nchi kwa urahisi zaidi” alibainisha na kuongeza.
Faida
nyingine kwa mujibu wa afisa huyo wa TCRA ni kurahisisha utatuzi wa migogoro
ihusuyo usajili wa majina chini ya kikoa cha.tz ambapo ni rahisi zaidi kutatua
migogoro hiyo hapa nchini kwa sheria na kanuni za Tanzania, tofauti na majina
ya kikoa yanayosajiliwa nchi nyingine au kimataifa; aidha kikoa cha .tz kinatoa
uthibitisho thabiti wa bidhaa za kitanzania kwa wateja mtandaoni na kuongeza
afua za usalama kwenye mtandao wa intaneti. Ni rahisi zaidi kudhibiti usalama
wa huduma za kimtandao ikiwa tovuti imesajiliwa kwa jina la kikoa cha .tz
Usajili wa huduma za mtandao wa intaneti kwa kutumia kikoa cha
.tz pia, unawezesha kuwasiliana, utoaji huduma, kurahisisha biashara kwa sekta ya umma na
binafsi. Matumizi ya dot tz ni rahisi na panapotokea tatizo la kiufundi muhusika
anapiga simu katika ofisi za TCRA na tatizo hutatuliwa papohapo tofauti na
vikoa vingine ambavyo huhitaji kufuata mlolongo uliowekwa kwa ajili ya utatuzi
wa tatizo husika ambao huchukua muda kutatuliwa.
****************=====****************

0 Comments
Post a Comment