Makamu Mwnyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata kwaajili ya Uchaguzi Mdogo wa udiwani kwa Kata 14 za Tanzania Bara unaotaraji kufanyika Julai 13,2023.






Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewaelekeza Wasimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha kwamba watendaji wa vituo vya uchaguzi wanapatikana kwa kuzingatia vigezo ili kuwe na ufanisi na weledi kwenye uchaguzi.

Maelekezo hayo yametolewa na Makamu Mwnyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifunga mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata yaliyofanyaka jijini Tanga kuanzi tarehe 19 Juni, 2023.

Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 14 za Tanzania Bara ambao umepangwa kufanyika tarehe 13 Julai, 2023.

“Kuhusu ajira za kuwapata watendaji wa vituo, tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hii muhimu, jambo hili limekuwa likisisitizwa tokea siku ya kwanza ya mafunzo kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni. Kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika kuitekeleza,” amesema Jaji Mbarouk.

Amesisitiza kwamba mafunzo kwa ajili ya watendaji hao wa ngazi ya vituo yafanyike kwa ufanisi na weledi katika tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.

Jaji Mbarouk mesema kwamba mafunzo hayo kwa watendaji wa vituo ni muhimu kwa kuwa yanalenga kuwajengea uwezo ili waweze kufahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo wakati wa uchaguzi.

“Ni matazamio ya Tume kwamba baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi wa tarehe 13 Julai, 2023,” alisema Jaji Mbarouk.

Kata zinazotarajiwa kufanya uchaguzi mdogo ni pamoja na Ngoywa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kalola iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Sindeni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kwashemshi iliyopo Halamshauri ya Wilaya ya Korogwe, Bosha iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mahege iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Bunamhala iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Nyingine ni, Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mnavira iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Kinyika iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Magubike iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Mbede iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.