Na Mwandishi Wetu Arusha, Oktoba 25, 2023
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutoa elimu kwa umma na kuhamasisha juu ya usalama mtandaoni, ikizingatiwa kwamba mwezi huu wa Oktoba ni mwezi wa Usalama Mtandaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha wakati akiwasilisha Taarifa ya Mwenendo wa Sekta ya Mawasiliano, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, alisema kuwa TCRA inaendelea na kampeni ya "Futa Delete Kabisa", ambapo inawakumbusha wananchi kuepuka kusambaza taarifa zozote zile zisizo za uhakika na za uchochezi.
Dkt. Bakari aliwasisitiza wananchi kuwa, pale ambapo wanapokea ujumbe wa kitapeli au simu ya kitapeli kwenye simu zao, watumie namba 15040 kutoa taarifa. Pia aliwakumbusha kuwa, usaidizi ambao mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu anapaswa kupokea kutoka kwa mtoa huduma wa mawasiliano ni kupitia namba 100 pekee.
"Unapopata taarifa ambayo huna uhakika nayo, ni taarifa ambayo haiendani na mila zetu, ni taarifa ya hovyo, unatakiwa kufuta na kudelete kabisa, kwa sababu unapoisambaza unafanya kosa na inaweza kukuletea matatizo, futa delete kabisa," alisisitiza Dkt. Bakari.
Kuhusu Kampeni ya uelimishaji wadau wa sekta ya mawasiliano inayohusu upatikanaji wa leseni za mawasiliano Kidijitali, Dkt. Bakari alisema kuwa, TCRA imeboresha namna wanaohitaji leseni hizo wanaweza kuzipata kupitia mtandao katika Jukwaa la mtandaoni liitwalo ‘Tanzanite Portal’ ambalo linapatikana kwenye tovuti ya TCRA.
Dkt. Bakari aliwasisitiza watoa huduma wote wa Mawasiliano, kuhuisha leseni zao, kwa mujibu wa Sheria na taratibu. Pia aliwasisitiza wananchi kuhakikisha wakati wote wanapohitaji kupokea huduma za sekta ya mawasiliano wahakikishe wanazipata kutoka kwa watoa huduma wenye leseni ya TCRA.
"Wananchi wahakikishe wanapokea huduma kutoka kwa mtoa huduma ambae ana leseni hai, kwa sababu kuna watoa huduma ambao wanaendelea kutoa huduma wakati leseni yake hajahuisha," alisisitiza Dkt. Bakari.
Wachambuzi wa masuala ya mawasiliano wameipongeza TCRA kwa kazi nzuri inayofanya katika kuelimisha wananchi kuhusu usalama mtandaoni na upatikanaji wa leseni za mawasiliano Kidijitali.
Bi. Asha Mlay, mkazi wa Arusha, alisema kuwa, kampeni ya "Futa Delete Kabisa" ni muhimu sana kwani inawasaidia wananchi kuepuka kushirikishana taarifa za uongo na za uchochezi mtandaoni.
Bw. John Mwita, mtoa huduma wa mawasiliano jijini Arusha, alisema kuwa, mfumo wa Tanzanite Portal ni rahisi kutumia na umewawezesha watoa huduma wa mawasiliano kuhuisha leseni zao kwa haraka na kwa urahisi.
Kwa upande wao Wanahabari wa mtandaoni JUMIKITA kupitia kwa Mwenyekiti wao Shaban Omary Matwebe waliweka bayana kwamba utaratibu wa TCRA kuanzisha Jukwaa la pamoja la leseni mtandaoni ‘Tanzanite Portal’ umewarahisishia pakubwa watoa huduma ya maudhui kwenye mtandao kupata huduma kwa haraka huku gharama za leseni zikiwa zimepunguzwa kwa asilimia hamsini.
“lakini kipekee kwa sababu Serikali imeweka njia nyepesi ya kuapply (kuomba) leseni kupitia mtandao maana yake ni nini, ni wewe tu kuwa na vile viambatanisho, kitambulisho chako cha NIDA na karatasi nyingine chache basi unaomba unapata, tunapongeza sana TCRA kwa jambo hili,” alisisitiza Matwebe.
Mamlaka hiyo iliyoasisiwa miaka 20 iliyopita imepewa jukumu la kusimamia sekta ya mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imekuwa na utaratibu wa kuchapisha taarifa ya mwenendo wa sekta ya mawasiliano katika kipindi cha kila Robo ya mwaka wa Fedha ili kuhakikisha wadau wa sekta wanapata fursa muhimu ya kwenda sambamba na mageuzi na maboresho yanayotokea kwa kasi katika sekta ambapo kwa Robo ya Kwanza ya mwaka wa Fedha 2023/2024 sekta ya mawasiliano imeendelea kukua kiidadi, kiteknolojia na kiusimamizi.
0 Comments
Post a Comment