Taasisi isiyo ya Kiserikali ya TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vimefanya uchambuzi wa bajeti yenye mrengo wa Kijinsia katika ukumbi wa halmashauri mgeni rasmi akiwa ni Kaimu Mkurugenzi Aliko Mbuba.
Katika hotuba yake Mbuba amesema halmashauri imekuwa ikishirikiana vema na TGNP mara zote walizoshauri halmashauri imekuwa ikichukua hatua mbalmbali hasa kutenga bajeti katika masuala ya afya,elimu,maji na uwezeshaji kiuchumi.
Rose Mwalongo mshauri kutoka TGNP amesema mrejesho umekuwa mzuri hususani katika sekta za afya,maji na elimu ambazo zimelenga mrengo wa kijinsia sanjari na msisitizo wa ushirikishwaji kwa wanaume.

Mwalongo amefurahishwa na mabadiliko makubwa katika bajeti ya halmashauri ya Mbeya kwani wamekuwa wakitenga fedha kwa ajili taulo za watoto wa kike hali iliyoongeza ufanisi katika masomo ambapo mahudhurio kwa watoto wa kike yameongezeka.





Naye Mhandisi Evetha Nzogela kutoka RUWASA Wilaya ya Mbeya amesema wao katika sekta ya maji wamezingatia mrengo wa kijinsia ili kuyafikia malengo ya serikali hususani ongezeko la upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 85 ifikikapo mwaka 2025.

RUWASA imekuwa na mpango endelevu hasa kwenye vijiji kwa kujenga vioski vya maji karibu sanjari na kuwahimiza watu kuingiza maji majumbani ili kuondoa migogoro ya ndoa iliyokuwa ikitokea kutokana na wanawake kutafuta huduma ya maji mbali na makazi yao.

Aidha Zawadi Merere ni Mwakilishi wa Kikundi cha Taarifa na Maarifa kutoka Kata ya Tembela ameishukuru TGNP kwa kuwaongezea ujuzi wa kuyapambanua mambo ikiwemo uchambuzi wa bajeti na kujiamini ambapo kwa sasa huduma za afya zimezidi kuimarika katika vijiji mbalimbali katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya zoezi lililosaidia kupunguza vifo kwa mama na mtoto.

Kaimu mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt Mary Mwakyembe amesema changamoto mbalimbali zimetatuliwa zikiwemo za upatikanaji wa dawa pia kadi za kliniki kwani kwa sasa hakuna tena uhaba wa kadi hizo ambapo zahanati zinaruhusiwa kuagiza bohari ya dawa(MSD).

Hata hivyo changamoto ya upungufu wa watumishi sekta ya afya limepungua kwani kila mwaka wamekuwa wakipokea watumishi wapya kupitia serikali na Wizara ya Afya.

TGNP imezidi kuvijengea uwezo vikundi mbalimbali vya taarifa na maarifa mbali kupinga ukatili wa kijinsia imewajengea uwezo wanawake katika kugombea uongozi pamoja na uanzishaji wa miradi ya kiuchumi.