MHANDISI MARYPRISCA AKUTANA NA MADUDU MENGINE YA WAKANDARASI WA MAJI SENGEREMA,ATOA MAAGIZO MAZITO
Na Ripota wa Mbeya Yetu, Sengerema
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ameendelea na ziara yake ya kukagua Miradi ya Maji Mkoani Mwanza na kukutana na madudu mengine ya Wakandarasi wa Miradi ya Maji Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Mhandisi Maryprisca ameshuhudia hali ya kusikitisha kutokana na
mkandarasi Mzawa kushindwa kutekeleza mradi wa maji kwa wakati na hivyo kuagiza
kutowavumilia Wakandarasi wa aina hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Maji vijijini
(RUWASA) Sengerema, Mhandisi Cassian Wittike amesema mradi huo ulikuwa
ukitekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya D4N Construction Limited ya
Wilayani Kahama ambaye ameshindwa kuukamilisha kwa mujibu wa mkataba wake.
"Mradi huu ni miongoni mwa miradi tuliyorithi kutoka kwa Mamlaka
za Serikali za Mitaa mwaka 2019 haukukamilika kutokana na uwezo mdogo wa
mkandarasi," amesema Mhandisi Wittike.
Asema kwamba mradi huo umeanza kutekelezwa tangu Desemba 2013 ambapo ulipaswa kukamilika Juni, 2014 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7.
"Mkandarasi aliyepewa jukumu ameshindwa tumeuchukua mardi na kuanza kutekelezwa na wataalam wa RUWASA Sengerema kuanzia mwaka 2019 na sasa hivi tupo kwenye majaribio na umeanza kutoa maji", amebainisha Mhandisi Wittike.
Kufuatia maelezo hayo na hali halisi ya mradi aliyoishuhudia,
Naibu Waziri Mahundi amesisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi mzembe
na badala yake atanyang'anywa mradi na atawekwa kwenye orodha ya wakandarasi
ambao hawana sifa ya kukabidhiwa kutekeleza miradi ya maji kote nchini.
Mhandisi Mahundi amesisitiza kwamba Serikali imeonya wakandarasi wote wenye tabia ya kutumia fedha wanazolipwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji badala yake wanaipeleka kwenye masuala mengine yasiyohusiana na mradi.
"Wakandarasi mnapaswa kutambua fedha mnayolipwa ni kwa
ajili ya kujenga miradi na siyo kufanyia matumizi mengine sasa bahati mbaya
huwa fedha hii mnaipeleka kwenye matumizi tofauti na hapa ni lazima mshindwe
kutekeleza miradi kwa ubora uliokusudiwa," amesema Naibu Waziri wa Maji.
0 Comments
Post a Comment