TAASISI YA LSF YATOA ELIMU YA MIKOPO MTAA KWA MTAA

Na Mwandishi Wetu

Taasisi Isiyo ya Kiserikali LSF iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji TEKU imeanza kutoa elimu kwa wananchi katika vituo vya Mabasi ili kuwajengea uwezo wananchi kuepukana na mikopo umiza inayotolewa na Taasisi zisizosajili rasmi.

Meneja Miradi LSF Agripa Senka kwa nyakati tofauti eneo la kituo cha Mabasi Uyole na Kabwe amesema wananchi wengi wamejiingiza katika mikopo umiza bila kujua masharti ya mikopo, hivyo kujikuta matatani kwa kupoteza mali zao kama vile Nyumba,Magari,Fedha na Mashamba.

Amesema kuwa mikopo hiyo haishirikishi wenza kama vile mke na mume hivyo kusababisha migogoro katika ndoa.

Naye Wakili wa Taasisi hiyo Martha Gwalema amesema kampeni hiyo imepata mafanikio kutokana na wananchi wengi walioguswa na mikopo umiza wamejitokeza kuomba msaada wa kisheria na baadhi yao wamerejeshewa mali zao kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU.

Kwa upande wake wakili Ezelina Mahenge ambaye ni Mkufunzi wa mafunzo ya mikopo, amewaasa wananchi kubla ya kuingia mikataba ya mikopo wanapaswa kusoma kwa makini mikataba na ikiwezekana kuwatumia wanasheria katika vituo mbalimbali vilivyopo katika kila kata Jijini Mbeya.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza akiwemo Subira Mwalwembe mkazi wa Ilemi Jijini Mbeya amesema wanawake wengi ndoa zao zimeyumba kutokana na kukopa shilingi elfu hamsini tu na kujikuta akilipa shilingi Milioni Moja.

Ameiomba Taasisi kuendelea kutoa elimu ili Wananchi wazidi kupata uelewa.


Zaidi ya wananchi laki mbili wamefikiwa na Taasisi ya LSF kwa kipindi kisichozidi miezi 6 huku wengi wakielewa namna ya kuanza kukopa mikopo yenye tija.