Shirika la Umeme TANESCO Mkoani
Songwe limetekeleza agizo la Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo kwa
kufunga Transfoma kwenye Kiwanda kipya cha Kukoboa Kahawa cha Majinjah Coffee
Curing Limited kilichopo Igamba Wilayani Mbozi Mkoani Songwe.
Agizo hilo limetekelezwa ikiwa
imepita wiki moja tu baada Katibu Mkuu Chongolo kuipa siku 21 TANESCO kuhakikisha
Transfoma hiyo inafungwa kiwandani hapo ili kusaidia mwekezaji kuanza
uzalishaji ambao utachangia ajira kwa wananchi na kuongeza uchumi wa Taifa.
Awali Msimamizi wa miradi wa Kampuni
ya Majinjah Logistics Mhandisi James Mgeni alitoa maelezo mbele ya Katibu Mkuu
juu ya changamoto za kiutendaji zinazosababisha kiwanda kuchelewa kuanza
usalishaji kwa kukosa Transfoma.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo
katika hitimisho la ziara yake Mkoani Songwe alitoa maagizo na kusisitiza
Shirika la Umeme TANESCO kupeleka Transfoma kiwandani hapo ndani ya siku 21 ili
mwekezaji Majinjah Coffee Curing aanze uzalishaji.
Kwa upande wake Mwekezaji Alinanuswe
Kabungo (Mzee Majinjah) ameshukuru jitihada za kiutekelezaji zinazosimamiwa na
CCM na kuhamasisha utendaji uliotukuka uliofanywa na Shirika la Umeme TANESCO
Mkoani Songwe.
Mzee Majinjah amemshukuru kipekee
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwa kuona umuhimu wa uwekezaji ambao unasaidia
kuliletea tija Taifa kiuchumi sanjari na kuongeza ajira kwa wananchi.Kiwanda hicho kipya cha Majinjah
Coffee Curing kipo katika kijiji cha Mawanga Kata ya Igamba wilayani Mbozi
Mkoani Songwe kina Uwezo wa kukoboa tani 72 kwa siku na teknolojia ya kisasa itakayomrahisishia
mkulima kukobolewa kahawa yake kuweka madaraja na kufanya usindikaji.
0 Comments
Post a Comment