WANANCHI WALIPISHWA SHILINGI 200 KUVUKA DARAJA LA MITI

Wananchi wa kijiji cha Manda wilaya ya Nywang’wale mkoa Geita wameiomba serikali kuwajengea daraja jipya baada ya daraja la awali walilokuwa wakilitumia kusombwa na maji wakati wa mvua Januari mwaka huu.

Kubomoka kwa daraja hilo kulisababisha kukatika kwa mawasiliano kutoka vijijini kuelekea makao makuu ya wilaya na kulazimika kutumia daraja la miti ambalo hutozwa shilingi 200 ili kuweza kuvuka.

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde wakati akikagua eneo hilo wamesema kuwawamekuwa wakipata mateso kutokana na kukosekana kwa daraja kuvuka upande wa pili kwa ajili ya kufuata huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za afya na shule.

Akiwawakilisha wakazi wa Jimbo la Nyang’wale Mbunge wa jimbo hilo Husein Nassor Amar ameiomba serikali kusaidia ufumbuzi wa tatizo hilo ili kupunguza kero kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde amemuagiza Meneja wa TARURA Wilaya Nyang’wale Benjamin Mkalava kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika kabla ya msimu wa mvua kuanza.

‘’Mkimaliza kujenga mniletee taarifa, mpige picha tuone watu wanapita ili tusiendelee kumwangusha Rais wakati wa utekelezaji wa ilani ya CCM’’.