Na Rashid Mkwinda, Mbeya Yetu Tv

Wamiliki na Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii wa Mikoa ya Mbeya na Songwe wametakiwa kuunda umoja utakaowawezesha kupaza sauti zao kuifikia jamii kwa uwanda mpana.

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa juma katika kikao cha pamoja kilichowahusisha baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii Mikoa ya Mbeya na Songwe na Watendaji wakuu wa Jamii Media kutoka Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Tughimbe Jijini Mbeya.

Akizungumza katika mjadala wa pamoja Mkuu wa miradi wa Jamii Media Gervas Mahimbi amesema wazo la kuanzisha Umoja wa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii limelenga kuwakutanisha na kupaza sauti ya pamoja kama chombo kinachotambulika rasmi.

‘’Tumekwisha sajili Tanzania Online Media Network,hiki ni chombo rasmi kwa wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii kitakuwa ni sauti inayokidhi mahitaji,kwa kuzingatia weledi na maadili’’amesema Mahimbi.

Aidha kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media Mike Mushi amesema katika utafiti ambao Jamii Media imefanya wamegundua kuna upungufu katika uendeshaji na ubunifu jambo linalosababisha uendeshaji wa mitandao ya kijamii isiwe na tija.

Amesema kupitia Tanzania Online Media Network waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii ili watanufaika kwa kupata mafunzi ili kubadilisha taswira na mtazamo kuhusu mitandao ya kijamii kwa wananchi.

Mushi amewataka waendeshaji wa mitandao ya kijamii kutembelea tovuti www.onlinemedia.co.tz ili kupata taarifa zinazohusu Tanzania Online Media Network kwa wakati.




''Tukiwa pamoja sauti zetu zitasikika,tutaendesha mitandao kwa tija jamii itanufaika na sisi''


Baadhi ya Washiriki wa kikao hicho cha pamoja kati ya mikoa ya Mbeya na Songwe wameelezea changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa mitandao ya kijamii kila siku.