MBUNGE MH SUMA FYANDOMO AWATIA MOYO WANAWAKE WA MKOA WA MBEYA



Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Suma Fyandomo amewatia moyo akina mama na kuwataka kujitokeza katika shughuli zote wanazodhani kuwa zinafanywa na wanaume pekee.

Fyandomo amesema kuwa Mwanamke ndio nguzo ya familia na anatakiwa ajitambue kuwa yeye ndiye nguzo ya familia kwa kuwa jambo lolote linaloihusu familia mwanamke ndiye anakuwa mtu wa kwanza kutolea majibu.

Amesema wakati wa kuwasubiri wanaume kutekeleza majukumu ya kifamilia zimepitwa na wakati ni vyema akina mama kusimama kidete katika kusimamia familia ili kusaidia sehemu ya majukumu ya wanaume.

Mbunge Suma Fyandomo amesisitiza kuwa majukumu yote yanayofanywa na mwanaume katika kusimamia na kuitunza familia yanaweza kufanywa na mwanamke hivyo ni vyema wanaume wakapunguziwa mzigo ili sehemu inayobaki itekelezwe na mwanamke.

Kadhalika ametoa wito kwa akina mama kujishughulisha na ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia asilimia 10 ya mikopo inayotolewa na Halmashauri  kwa makundi ya akina Mama Vijana na Wenye ulemavu.

Fyandomo ni mmoja kati ya Wabunge watatu viti maalumu wanaowakilisha mkoa wa Mbeya akiwemo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi na Bahati Ndingo anayewakilisha wazazi Taifa.